Quantcast
Channel: Free Thinking
Viewing all articles
Browse latest Browse all 3176

Moja ya sifa za Kikwete ni kulea ufisadi

$
0
0
  • and Tanzania president, Jakaya Kikwete (Left), promotes Rostam ...
Rais Jakaya Kikwete karibuni atatundika jezi kama rais wa nchi baada ya kuitawala Tanzania kwa vipi viwili vyenye utata. Hata hivyo, atakumbukwa kwa hisia tofauti kulingana na anayemtathimini alivyouona utawala wake. Kwa waliofaidika na utawala wake –hasa mafisadi –Kikwete atakumbukwa kama rais aliyewakomboa. Kwa wananchi wa kawaida maskini wanaoendelea kuumizwa na ufisadi na kuparaganyika kwa uchumi, watamkumbaka Kikwete kama rais wa hovyo aliyewazamisha zaidi kwenye mateso na mahangaiko bila sababu za msingi.  Rejea kunyamazia ufisadi wa kutisha kama vile escrow ukiachia mbali kutumia fedha za umma vibaya kwa kuizunguka dunia akiandamana na kila watu wenye kutia shaka ambao mara nyingi walifanywa siri.
Pia Kikwete atakumbukwa kama rais ambaye angeweza kujisemea lolote bila kujali athari zake. Rejea alivyosema kuwa wanafunzi wa kike wanaopachikwa mimba ni kwa sababu ya kiherehere chao. Sijui binti zake wangekuwa waathirika kama angeyasema haya.
Nadhani seriali yake itaingia kwenye vitabu vya historia ya Tanzania kama rais aliyesimamia ufisadi wa kutisha mwingine akituhumiwa moja kwa moja kuushiriki bila kutoa maelezo au kukanusha.  Rejea kashfa ya EPA ambayo inasemekana fedha zake ndizo zilimuwezesha kuwashinda wapinzani wake na kuingia madarakani akaendeleza mchezo ule ule. Rejea kashfa ya hivi karibuni ya escrow ambapo watuhumiwa wakubwa licha ya kuwa nje wakitanua, wengine wamesafishwa na ikulu ya Kikwete huyu huyu.
Kikwete atakumbukwa kama bingwa wa kutoa ahadi lukuki za kila aina asizitekeleze. Yako wapi maisha bora kwa wote yaliyogeuka bora maisha kwa wengi hasa ambao hawako karibu naye wala kuwa kwenye utawala wake.
Moja ya mambo ambayo atakumbukwa kwayo Kikwete ni kashfa zilizamisha mabilioni ya shilingi. Kashfa inayovuma kwa sasa –kama ilivyoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ni ya serikali kuendelea kuwalipia maafisa wake walioko ughaibuni hata baada ya kustaafu. Je kwanini serikali ilifanya hivyo na kwa faida gani kama hakuna namna?
 Kimsingi, hawa ni wahalifu wanaopaswa kufungwa kwa kuhujumu taifa. Na isitoshe, wengi wa waliofichwa huko ughaibuni ni ndugu, jamaa au watoto wa wakubwa ndiyo maana serikali inatenda jinai hii kwa umma maskini wa watanzania. Wengi wameteuliwa kwa vigezo vya ajabu ukiachilia mbali kwa kificho kikubwa. Hivi watoto kama wa Edward Lowassa, Pius Msekwa, kweli wameteuliwa kwa vigezo gani zaidi ya majina ya wazazi na mitandao ya wazazi wao?
Kichekesho ni pale waziri anayesimamia wizara hii Bernard Membe kuutaka urais wakati anasimamia na kubariki ufisadi. Kama ameshindwa kusimamia wizara moja ataiweza nchi? Nadhani hiki ni kigezo kuwa Membe hafai kabisa kuwa rais kwa vile ameonyesha wazi anavyoshabikia ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma. Taarifa ya CAG inabainisha kuwa jumla ya Sh 543.7 milioni zilitumika kuwalipa watumishi wa balozi za Tanzania waliostaafu, waliokuwa wakifanya kazi bila kuwa na mikataba kutokana na changamoto za malipo ya kurejeshwa nyumbani. Balozi ziliozoongoza kwa wizi huu ni zile za Kinshasa (DRC), Maputo (Msumbiji), Ottawa (Canada) na Washington DC (Marekani). Ajabu ya maajabu, aliyekuwa balozi wa Tanzania Washington Liberata Mulamula alipandishwa cheo hivi karibuni na kuwa katibu wa wizara pamoja na kutajwa kwenye kashfa hii moja kwa moja. Kesho utasikia Shamim Nyanduga (Maputo) na Hemed Mgaza (Kinshasa) wamepandishwa vyeo. Kwa ubalozi wa Ottawa wengi walishuku pale alipoteuliwa mtuhumiwa wa utesajiwa Dk. Steve Ulimboka Jack Zoka.   
Nadhani yote haya ni matunda ya uteuzi wa kujuana na kulipana fadhila ambao kimsingi, unadhoofisha uchumi wa taifa bila sababu za msingi. Kwa sasa Tanzania chini ya Kikwete inajiendesha au tuseme inaendeshwa kihovyohovyo na umma haustuki na kuchukua hatua.
Kikwete atakumbukwa kama rais aliyetamka wazi wazi kuwa ana orodha za wahalifu mbali mbali kuanzia mafisadi, wauza unga, majambazi lakini akasita kuwachukulia hatua pamoja na kupewa majina yao. Kwanini na ana faida gani nao? Nani anajua? Hakuna sehemu aliponiacha hoi Kikwete kama mkuteua Hilda Gondwe kwenye Tume ya Maadili ya Viongozi wakati mhusika anatuhumiwa kujipatia gari la serikali aina aina ya Toyota Land Cruiser VX iliyokuwa imenunuliwa miaka mitatu kabla kwa shilingi 155,000,000 kwa shilingi milioni moja na nusu tu huku akiusababishia umma hasara ya shilingi 149,000,000. Hata angekuwa Obama rais wa taifa tajiri asingemteua mtu huyu licha ya kutokumfikisha mahakamani. Huyu ana maadili gani wakati ni bingwa wa kupiga madili? Inaonekana hii ndiyo aina ya watu anayoitaka Kikwete kwa sababu anazojua mwenyewe.
Kitu kingine ambacho Kikwete atakumbukwa kwacho ni kujenga barabara ambazo hata hivyo hazikidhi viwango wala kulingana na kiwango cha fedha kilichotumika kuzijenga.
Pia Kikwete atakumbukwa kama rais ambaye serikali yake ililitumia vibaya jeshi la polisi kiasi cha kusababisha vifo na mateso ya watu wengi. Rejea mauaji ya mwanahabari Daud Mwangosi na kuteswa kwa daktari Ulimboka na mwandishi wa habari Absalom Kibanda.
Pia Kikwete atakumbukwa kwa kuwa rais wa kwanza kuamuru katiba aindikwe upya lakini akaisaliti na kutaka kupandikiza yake yenye kulinda mafisadi huku akipuuzia mawazo na maoni ya wananchi ukiachia mbali kutumia wahuni kumtisha aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Kukusanya Maoni, jaji Joseph Warioba.
Si rahisi kuorodhesha mambo mengi ya hovyo ambayo Kikwete atakumbukwa kwayo. Hata hivyo, kuna funzo toka kwenye utawala wa Kikwete kuu likiwa ni kwamba watanzania wasirudie makosa kuchagua mtu kwa kuangalia sura, ahadi na ubobeaji wake katika usanii wa kisiasa.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 27, 2015.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 3176