Pamoja na kuupiga mma kiasi cha kujisahau, sijasahau kaya yangu. Nafahamu sana tu. Nakumbuka sana tena kwa moyo wote na akili zangu zote na kwa uwezo wangu wote. Kaya yangu ni maskini wa kutupwa ambapo mzito wetu aka rahisi aka prezo aka mnene aka baba Riz anasifika kwa kuizunguka dunia akibomu ili angalau wabongo waende wee koma! Nikikumbuka alivyokuja na sera na kauli yake mbinu ya ANGUKA ambayo walevi hawakuipata, natamani kujinyotoa roho ili nisiendelee kushuhudia haya makufuru na mazabezabe ninayoshuhudia.
Najua viherehere wa bwana mkubwa wanasema, “Sasa tumempata huyu chizi mlevi kwa kusema eti sera ya muungu wetu ni ANGUKA.” Wala msijisumbue. Maana ya ANGUKA ni simpo. Ari mpya, Nguvu Mpya na Kasi mpya katika lolote unalofanya. Ukitumia sayansi hii ya ANGUKA lazima uangushe wale uliowaahidi hayo maanguko hapo juu. Hayo tuyaache. Humu si mwake leo. Na kama si kuheshimu sheria na huruma yangu, huenda ningetoka hapa na kwenda kula nyama ya mshenzi huyu anayeibia kaya yangu halafu na kuanza mashauzi ya kipuuzi. Shame on you! Don’t you know that we know you are but a con man? We know everything. If you go on vomiting like that we’re going to teach you a lesson.
Wahenga walisema. Ukishangaa ya mlevi utaona ya mgema. Si nikiwa ndiyo nimerejea kutoka kupata kanywaji si nilikutana kuku wawili wakigombana tena kwa sauti za juu. You know what. Baada ya kukaa na kuwasikiliza kwa muda niligundua kuwa kumbe wale kuku walikuwa mke na mme wakigombea mambo ya unyumba na tabia ya jogoo kuwa na nyumba ndogo kibao. Baada ya kuupata ukweli sikuona haja hata ya kuwasuluhisha. Niliachana nao nikijisemea moyoni, “Mkikutana na wezi wa kuku huenda mtatia akilini.”
Baada ya kushangaa ugomvi wa kuku si nilipata baba lao. Baada ya kutia timu home si mama Domo Kubwa akanipa stori iliyofanya hata ugomvi wetu niliokuwa nimeukimbia asubuhi wa kumwibia njuluku utoweke. Alinipa kisa cha nshomile mmoja aitwaye Jemus Rugemaaalira aliyesema eti madafu bilioni 120 ni vijisenti vya ugoro. Alisema, “Mume wangu nilikuwa najua wewe ndiwe kibaka wa mibaka kayani mwetu kumbe uongo.”
Kabla ya kuendelea nilimuingilia nikisema, “Mama Domo chunga mdomo wako tusitoane ngeu bure. Wewe ni kuniita mimi mumeo kibaka wa mibaka wakati mibaka yenyewe unaiona ikiwa kwenye ulaji?” Hebu niombe msamaha kabla sijajinyotoa roho ukaishia kuwa mjane usawa huu ambapo unanihitaji kwa mengi.”
Kasheshe na mshikemshike wa kimbembe viliishaje? Si kazi yako kujua. Maana utapata umbea wa kuwapa washirika na washikaji zako bure.
Kwanza, sikumuani bi mkubwa kwa vile tulivyopigika kusikia ngurumbili akisema eti mabilioni ni vijisenti vya ugoro bila shaka mdudu mtu huyu atajhitaji kuchunguzwa bichwa lake. Hawezi kuwa mzima huyu. Kama ni mzima basi kichaa chake bado kichanga. Unashangaa huyu anayesema eti bilioni 120 ni vijisenti vya ugoro kwanza ana uchache kiasi gani? Je ameupataje? Je analipa kodi ya biashara zake uchwara za kutapeli hapa na kule?
Leo nina maya na mpuuzi mmoja aliyelewa fweza za wizi hadi akakufuru tena mchana kweupe. Hivi kama si kufuru ni nini kuita madafu bilioni 120 au dolari za KiObama 75,000,000 vijisenti tena vya ugoro? Huo ugoro ni aghari kiasi gani hadi kugharimu njuluku nyingi ambazo hata rais wako hawezi kupewa kwa mkupuo mmoja anapokwenda ughaibuni mara kwa mara kubomu? Nashauri huyu mjivuni nshomile awekwe ndani mara moja kabla sijajifunza ugaidi nikafa na mtu mie.
Baada ya bi mkubwa kunipa full story ya nshomile mjivuni niliingia porini kusaka habari zake ili lau nimjue na kama ikibidi kumchukulia hatua niwe namjua fika. Kwa vile mimi ni prof wa utafiti, haikuwa kazi ngumu kumfukua na kumpata mtu mwenyewe ambaye kumbe anatia shaka kulhali. Kwanza, niligundua kuwa huyu nshomile anayeita mabilioni vijisenti vya ugoro ni mtoto wa kapuku huko kwao. Nasikia baba yake alimsomesha kwa kulima vibarua kwa majirani zake na alikuwa akilalia ngozi ya mbuzi maisha yake yote hadi siku alipoanza kidato cha kwanza kwenye shule moja mkoani kwake ambayo nitaitaja baadaye.
Pia niligundua kuwa huyu jamaa alizaliwa akiwa tapeli. Alianza kutapeli vifaranga na vitu vingine vidogo vidogo kabla ya kupata elimu na kuitumia kuwaibia walevi.
Nilipokutana na walevi kujadili jambazi huyu anayejulikana kwa kuiingiza kaya kwenye migao na ulanguzi wa umeme kutokana na kampuni la kitapeli la IptL alilo nalo ubia chini ya mkampuni wake wa Vip Engmoneying vikiikamua kaya kwa kutofanya lolote. Jamaa huyu anafahamika alivyoshirikiana na matapeli wa kimalaysia kuiibia kaya. Mlevi mmoja alituacha hoi aliposema kuwa vyombo vya habari viliripoti kuwa huyu jamaa na majambazi wenzake walianzisha utapeli wao kwa jumla ya dola 50 lakini wakawa wanalipwa dola 100,000 kwa siku simply for doing nothing. Mlevi alituacha hoi aliposema kuwa hii kampuni ya Vip Engmoneying ni mali ya vigogo na huyu nshomile anatumiwa tu na wenyewe wenye mali ambao ni wazito kayani. Ndiyo maana huu utapeli wake akauita Vip Engmoneying. Huyu hana tofauti na akina Kagodamn walioiba pesa za EPA. Hawa kitaalamu tunawaita vyangudoa wa kiuchumi wanaoweza kutumiwa na fisadi yeyote mwenye madaraka. Wako tayari kujiuza kwa yoyote anayetaka kuwatumia atakavyo ilmradi mkono uende kinywani.
Katika research yangu niligundua kuwa huyu mjivuni nshomile na tapeli analindwa na dingi ambaye wakati mkenge na ujambazi huu ukisainiwa alikuwa waziri mkubwa wa wizara husika.
Baada ya walevi kudurusu historia ya nshomile huyu, wametoa mapendekezo kwa wachovu kuchagua wapingaji kwenye uchaguzi ujao ili hawa mafisi na mafisadi wakamatwe na kunyongwa kwa kupigwa mipini kama mbwa aliyeiba mafuta ili kutoa somo kwa wengine.
Chanzo: Nipashe Machi 15, 2014.