Quantcast
Channel: Free Thinking
Viewing all articles
Browse latest Browse all 3175

Article 0

$
0
0
HAKUNA ubishi. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeingiliwa au tuseme kuvamiwa na kansa mbaya.
Hakuna kitu kinakitafuna chama hiki kama mdudu wa kupenda madaraka huku wanaoyatafuta wakiwatumia makada wa chama sehemu mbalimbali kuwapigia kampeni jambo linalosababisha migongano na hata malumbano yanayokiua chama taratibu.
Hali ni mbaya sana. Watu wamefikia kuvuana nguo hadharani kuhakikisha yule “wanayemtaka”, huku naye akiwataka na kuwatumia nao wakimtumikia anapita hata kama ni kwa watu wazima kufanya mambo ya kitoto kama kuvuana nguo hadharani.
Ni bahati mbaya kuwa CCM imeishiwa na kufilisika kiasi cha kutokuwa na kiongozi mwenye uthutubu wa kukaripia mitandao hii inayodhoofisha na kuua chama.
Asikudanganye mtu. Wote sasa ni sawa na kambale. Wana sharubu, tena ndefu sana. Mitandao ya kifisadi, kiulaji na kimaslahi imechukua nafasi ya chama kiasi cha kukiangamiza taratibu kama kansa inavyoonekana na kila mtu ana mtu wake na maslahi yake.
Hata Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete naye yumo kiasi cha kuhojiwa. Naye ana mtu wake anayeweza kulinda maslahi yake. Haya si maneno yangu. Rejea karipio la Malecela aliyekaririwa hivi karibuni akisema: “Kinachonishangaza ni ukimya wa viongozi wa juu wa chama, akiwemo Mwenyekiti wa chama wa taifa, Rais Kikwete. Naitaka Sekretarieti ya CCM kutafakari, kumjadili kwa kina na kumwajibisha Lowassa, ikiwezekana atimuliwe uanachama.”
Mtifuano wa Malecela na Mgeja unanikumbusha kisa cha ugomvi wa washirikina waliokuwa wakigombea kila mtu na kinyago chake ndicho kiabudiwe hadi wakataka kutoana roho ilhali vinyago vikiwa salama.
Mwisho wa yote, walipogundua kuwa vinyago vyao havina lolote wala maana, waliamua kuvichoma moto na kumtafuta Mungu wa kweli. Je, Malecela na Mgeja watafikia hatua ya kuachana na mitandao na maslahi binafsi na kukirejea chama?
Hata hivyo, mchezo huu unaoelekea kusababisha mauti ya CCM ni ukombozi kwa Watanzania kama wataweka kumbukumbu. Pia mchezo huu ni faida kwa wapinzani kama wataamua kuvalia njuga haya madudu yanayofichuliwa na makada wa CCM wenyewe. Hakika mitandao imetandawaza kila aina ya sababu ya kuanza kuiaga CCM taratibu.
Leo hii ni zamu ya makada, Hamis Mgeja, Mwenyekiti wa CCM wa Shinyanga na Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu na Waziri Mkuu wa zamani, John Malecela. Baada ya Malecela kuita waandishi wa habari hivi karibuni na kukaripia tabia ya baadhi ya wana-CCM kuanza kutangaza kugombea urais hata kabla ya muda, amejichongea.
Malecela katika mkutano wake na waandishi wa habari alimtaja Edward Lowassa, mbunge wa Monduli na waziri mkuu aliyetimuliwa kutokana na kashfa ya Richmond wazi wazi kuwa hafai kuwa rais.
Siku mbili baadaye, Mgeja aliamua kumtolea uvivu Malecela jambo ambalo limetufanya kuuliza kulikoni Mgeja kumsemea Lowassa kana kwamba yeye ndiye wakili wake? Je, ametumwa au amejituma? Je, ana nini cha mno na Lowassa au ndiyo huku kutumiwa na kutumiana?
Mgeja alikaririwa akisema: “Huyu Malecela amesahau huko nyuma yeye alishawahi kutuhumiwa kuwa alipewa fedha kutoka nchi za Uarabuni na mpaka kubadilisha dini na kuitwa Jumanne ili aungwe mkono kupewa nguvu za kugombea urais.”
Laillah ila allah! Hatukuyajua haya na kama ni ya kweli basi kuna namna. Je, inakuwaje kwa Mgeja Muislamu aone kitendo cha Malecela kusilimu kama kitu kibaya kama hakuna namna? Pia Mgeja alisema kuwa Malecela alikataliwa na baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere hadi kumtungia kitabu.
Ajabu Mgeja huyo huyo sijui kwa kusahau kwa kutojua kuwa alitumia mfano mbovu, alisahau kueleza kuwa hata huyo Lowassa alikatiliwa na Nyerere huyo huyo.
CCM imeoza kwa rushwa jambo ambalo kumbe wananchi hawakujua. Kwani Mgeja aliongeza: “Malecela, Makonda na washirika wenzao wanajua kuwa wako baadhi ya wanachama wanagawa kalenda nchi nzima, wanagawa simu huku wakitumia magari ya serikali kugawa hizo takrima na inawezekana na wao pia walishawahi kuzipokea na wana-CCM wengi walishazipokea, hata mimi nilishapokea, mbona hizo hawasemi, nazo zinakivuruga chama?”
Je, hapa kinachogomba baina ya Mgeja na Malecela ni uchungu kwa chama au uchungu kwa mitandao? Je, Malecela ni kama Yusuf Makamba aliyeonyesha wazi wazi anamtetea na kumuunga mkono Lowassa? Wapo wanaosema kuwa anatumiwa.
Ni aibu kiasi gani kwa makada wa chama kuanza kuhongana na kutumiana kama nepi? Je, chama cha namna hii chenye uoza kuanzia kichwani hadi miguuni bado kina udhu na hadhi ya kuongoza taifa linalohitaji mkombozi toka kwenye rushwa ufisadi na majanga mengine ambayo CCM imeyasimamia na kuyatekeleza siku zote? Je, wananchi wanajifunza nini kutokana na vita hii ya mitandao maslahi?
Rushwa kwa sasa inatembezwa wazi wazi na waasisi madaraka wa ndani ya CCM. Watu wanauliza haya mabilioni yanayomwagwa yananunua nini na wahusika waliyapata wapi? CCM inanuka rushwa kiasi cha kutisha.
Rejea karipio la Malecela aliyekaririwa akisema: “Naomba niseme kuwa bila karipio au tamko la chama, hawa wanaotumia fedha hadharani kwa lengo la kutafuta umaarufu na ushawishi kwa vijana ili kupata madaraka, wataharibu misingi bora ya uongozi iliyowekwa na waasisi wetu ndani ya chama.” Kwa rushwa kama hii ya wazi wazi kumebaki kitu cha kuweza kuweka madarakani?
Watanzania wakifanya kosa wakarudia makosa kwa kuchagua chama fisadi na kinachoongoza katika rushwa wasijute wala kumlaumu mtu. Hawa watu wapo kwa maslahi yao fichi na si ya Watanzania. Laiti Watanzania wangewabana hawa watoa rushwa wakaeleza walikopata hizo pesa na wanataka kununua nini!
Tumalizie kwa nukuu ya Paul Makonda, Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi, aliyekaririwa akisema: “Lowassa amekuwa akiwatumia watu kusema ovyo, kwanza mwenyewe hana sifa ya kuwa rais wala kuwa amiri jeshi mkuu wa nchi, na kama wapo vijana hapa mjini wanaotaka fedha kwa haraka wamtafute.”
Kwa halli hii, Watanzania waliokuwa wemelewa mapenzi na imani kwa CCM wamejikuta mbele ya kinyago cha mpapure walichodhania ni Mungu. Kazi kwao. Wazee wazima wanafanya kile Waingereza huita, washing your linens in the agora.
Ukifikia hapo umeisha na kuishiwa. Watanzania wanapaswa kuifungisha virago CCM ili wenye uwezo waingie na kutawala. Hakuna tena sababu ya kuendelea kuiamini CCM isiyojiamini wala kuaminika.
Chanzo: Tanzania Daima Feb., 2014.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 3175