Wengi wa wapenda demokrasia, haki na usawa nchini watakuwa wameshangazwa na hata kuchukizwa na yaliyojiri hivi karibuni. Ni kuhusiana na sakata la kughushi; mbali na la uvamizi wa vituo ya Clouds. Hii ni baada ya kuachishwa kazi kwa aliyekuwa waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye. Hata hivyo, kosa lake halikuwekwa wazi ukiachia mbali kujengeka hisia kuwa kadhia hii ilitokana na Nape kuunda tume ya kuchunguza uvamizi wa vituo tajwa hapo juu. Japo rais hapaswi kuingiliwa kwenye mamlaka yake ya uteuzi au utenguzi, kuna haja umma kujulishwa hasa, ikizingatiwa mhusika alikuwa ameshikilia madaraka ya umma. Je kweli kosa la Nape ni kuunda tume kuwachunguza wateule wasioguswa?
Japo ni haki na mamlaka ya rais kuteua na kutengua, kuna haja, wadau yaani wananchi, kujulishwa kinachoendelea jikoni; kuepuka kujengeka dhana ya udikteta, upendeleo na upatilizaji kwa wenye mawazo tofauti. Umma unapaswa kujulishwa nani wanapaswa kuguswa na nani hawapaswi kuguswa hata watende makosa makubwa kiasi gani. Tanzania ni nchi ya kidemokrasia inayopaswa kuendeshwa kwa haki, kanuni, sheria na usawa bila kusahau katiba inayotamka wazi kuwa watanzania wote ni sawa na wana haki sawa.
Mengine yaliyoibuka kwenye kadhia tajwa ni matumizi mabaya ya vyombo vya dola. Inakuwaje mtu mmoja, tena asiye na stahiki kisheria kutumia vyombo hivi kwa maslahi binafsi na katika mambo binafsi kama ilivyokariri taarifa ya uvamizi wa Clouds? Mbali na hili, inakuwaje, kama taifa, tunaanza kuminya na kutishia vyombo vya habari ambavyo viko kikatiba na si kwa mapenzi ya mtu hata awe na mamlaka kiasi gani? Inakuwaje; wahusika wanashindwa kujua vyombo vya habari ni sauti ya wasio na sauti au voice of voiceless dhana nyepesi kabisa kujua? Rejea namna rais alivyokaripia na kutishia vyombo vya habari kuwa kama vinadhani vina uhuru, it is not to that extent au si kwa kiwango hicho. Haya si maneno ya rais anayefuata na kulinda katiba wala kuheshimu uhuru wa kiraia.
Katika kutishia na kuonya vyombo vya habari, rais alisikika akijigamba kuwa yeye ni rais anayejiamini na ambaye utawala wake hautokani na ushauri, usaidizi wala ushirika wa mtu yeyote. Kwani alipokwenda kuchukua fomu za kugombea urais, licha ya kutoshauriwa na yeyote, alikwenda peke yake. Hii ni kweli; japo sijui kama alijipigia kura na kushinda. Isitoshe, rais wa nchi anapaswa kuwa rais wa wananchi wote bila kujali tofauti zao. Hili, hakika, ndilo ambalo rais amekuwa akilihubiri; japo anaonekana kutolitenda. Kwa maneno ya rais, ni kwamba utawala wake ni wake binafsi. Je inawezekana taasisi kubwa na muhimu katika taifa ikadhibitiwa na mtu mmoja hata awe mjuaji kiasi gani? Urais kama, taasisi ni mkusanyiko wa vyombo vingi. Hivyo, unahitaji maelfu ya wananchi ili uweze kufanikisha malengo uliyokabidhiwa na wananchi. Hata wafalme huwa hawatawali peke yao pamoja na ufalme kuwa sawa na mali ya familia.
Japo simuonei huruma Nape kwa yaliyompata hasa ikizingatiwa alichangia kikubwa kuyaunda, nampongeza kwa kufia ukweli. Socrates (469 B.C. to 399 B.C), mwanafalsafa wa zamani wa Kigiriki aliyesifika kwa kupenda ukweli aliwahi kunena “do not be angry with me if I tell you the truth” yaani usinichukie ninapokwambia ukweli. Yesu naye alisema ‘tuitafute kweli; kwani itatuweka huru.’ Hii maana yake ni kwamba mtu anayechukia na asiyependa kweli si huru. Anahitaji uhuru hata kama ana uhuru wa kisiasa. Je hatuhitaji uhuru utokanao na kweli hata kama unawaudhi wenzetu tena wenye madaraka? Je kadhia inayomkabila mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Paul Makonda ya kughushi vyeti vya kitaaluma na kuvamia Clouds si ukweli tunaoutaka kama jamii ili, licha ya kutendeana haki kwa usawa, utuweke huru? Nani huyu mtumwa asiyependa kujua kweli imuweke huru? Je tunaweza kushindana na kweli na kuishinda tukawa salama kama jamii na taifa? Leo tutakwenda na falsafa ya Socrates tokana na mfano bora alioacha wa kuitafuta kweli hata kwa gharama ya maisha yake kama ilivyomtokea pale aliposhitakiwa kuwa alikuwa akiwaharibu vijana kwa mafunzo yake. Baada ya kuhukumiwa kunywa sumu aina ya Hemlock au Conium maculatum, Socrate alisema “yapo maarifa ya kweli na katika kujua hili hujui kitu.”
Tukirejea kadhia zetu hapo juu, nani hajui kuwa mengi yaliyojitokeza ni ya kweli? Nani hajui kuwa tumeanza kujenga taifa la watakatifu wasiokosea, wanaojua kila kitu na taifa la wasio na haki wala maarifa ukiachia mbali stahiki na haki ya kueleza mawazo yao? Nani huyu fedhuli anaweza kufunga mawazo? Je inawezekana? Ukijua hili jua hujui na kama hujui kuwa hujui basi hujui na utajua,
Tumalizie kwa mfano wa Socrates kuwa tusiogope kusema ukweli kwa kuhofia kufukuzwa, kunyamazishwa au kutishwa. Ukweli utabaki kuwa ukweli kuwa mambo yanavyokwenda, licha ya kuwa tofauti na mategemeo yetu, sivyo ndivyo. Uhuru wetu kama wana jamii una thamani na gharama ambavyo hakuna anayeweza kuvipoka huku nasi tukiangalia. Ama! Tanzania imefikia hapa!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.