Baada ya kushuhudia vimbwanga na vibwengo, visa, visasi, mikasa na makosa, kijiwe kimeamua kutia timu kwenye jiji la Koromije kule kwenye nchi ya Kusadika na Kuburuzika. Kinakwenda kule kumsaka mbaya wake aitwaye Bushit. Yote hii ni kutaka kuweka mambo sawa ili kaya iwe sawa iondokane na kubebana, kupatilizana na kuburuzana.
Akiwa amevalia kanzu yake na kofia ya tarabushi vya bei mbaya, Mgoshi Machungi leo kaja kinomi. Hata kabla ya kuamkua, Mbwamwitu anamchokoza “Mgoshi unaenda kuongeza jiko nini mbona leo umetisha hivi?”
Mgoshi anajibu “kama unaye mwai sina neno. Niko ai kamii. Si minaona niivyouamba. Isitoshe, napendeza na kuvutia kwa kia kinda na jiko au vipi jamani.si minipigie angau makofi kwa niivyojikwatua.”
Kama ada, anaamkua ‘asaamaeku jamia.” Tunajibu na anaendelea kula mic “wagoshi, hivi tinasemaje kuhusi hiki kitatange na kimbembe vinavyoeendee kwenye kaya?”
Mchunguliaji anajibu “yapo mengi yanaendelea kuanzia sanaa za kuwasaka na kuwanyaka wauza bwimbwi ambazo hata hivyo zimefunikwa na Bashiiit na Nipe Mapepe aliyetimliwa baada ya kutaka kuwagusa watakatifu hasa mwana wa pekee wa mfalme. Je unamaanisha lipi kati ya haya na mengine mengineyo?
“Mgoshi hapo umepiga kwenyewe. Ni kama uikuwa kwenye akii yangu! Kusema ue ukwei, hii kadhia ya kutishia vyombo vya umbea na kuindwa kwa Bashiiit vimenikea kiasi cha kuja na wazo kuwa tihamie huko Koomije tukakoome na kuchunguza ii tijue ukwei. Maana, inachanganya na kuudhi,” anajibu Mgoshi huku akimpa kikombe muuza kahawa ammwagie.
Mijjinga ambaye anatokea karibu na jiji la Koromije anakula mic “unadhani kuwa hata ukienda Koromije kusaka ukweli utapokelewa na kufanyiwa kazi? Mbona mkuu amesema atakufa na mtu wake na kumpatiliza yoyote atakayemgusa mwanae mpendwa? Hujitaki nini? Kamuulize Nipe Mapepe ndiyo ufanye hayo unayotaka kijiwe kifanye.”
Kapende anampoka mic na kuronga “nadhani wengi hawakumuelewa mkuu; wanamlaumu bila sababu. Kama nimemwelewa ni kwamba, hataki umbea na mambo ya kwenye mitandao. Anataka ushahidi wa kisayansi ndipo atumbue au vipi?”
Mipawa anamchomekea Kapende “nadhani hukumuelewa mkuu. Alichomaanisha ni kwamba wateule wasisemwe wala kukemea as long as yeye anawapenda na kuwakubali. Hivyo, hata tukienda kule na kuja na magunia ya ushahidi, tutazodolewa tu hasa ikizingatiwa kuwa mwenye mapenzi haoni. Mbona kwa Nipe Mapepe hakungoja kuletewa huo ushahidi wa kisayansi unaodhani ndiyo anaoutaka?”
Kanji anakatua mic “mimi ungana na veve. Kuu hapana taka hii teule guswa hata kama naua. Kuna kweli gani hapa natakiwa kama vote nasitaki yeye nasema kweli yote? Kama Kuu iko taka shahidi scientific kwanini nafukuza Pepe bila soma ripoti yake?”
Msomi anakatua mic “kimsingi, hapa Mkuu amefanikiwa kuua ndege wengi kwa jiwe moja. Kwanza, ametoa kauli za kuchanganya hata kuchanganyikiwa ikizingatiwa kuwa alifanya tofauti na anachohubiri. Pili, alitumia fursa hii kutoa vitisho kwa wote wanaodhani wanaweza kumkosoa wakati anajua kila kitu. Tatu, amethitibitisha ukweli kuwa ile sera ya kulindana ya chata lao bado ipo. Nne, amethibitisha kuwa maji yanaanza kuzidi unga kiasi cha kuchanganya. Tano, amemvua Nipe Mapepe gamba wakati akimwacha Bashiit mwenye magamba manene kibao ambayo kwa msemo wa mzee wa Vijsenti yanahitaji shoka na si kalamu. Je atamvua yule ampendaye?”
Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anadakia “chonde Msomi. Amvue ili iweje?”
Msomi anampuuzia na kuendelea “japo wazo la kijiwe kuhamia kufanya uchunguzi kule Koromije ni jema, je ukweli utakaopatikana utakubaliwa au kusulubiwa kama ule wa Nipe Mapepe? Je kuna masikio ya kuweza kuusikia wakati yaliyopo yameishajazwa vijiti? Nadhani hapa la kufanya ni ima kuingia mitaani ili kujua hii kaya ni ya nani, kunyamaza au kwenda kwa pilato kumshitaki mtuhumiwa. Vitendo vilivyotokea vimenikumbusha shujaa Chris Mtikisa. Angekuwa hai, kesi zingeishajaa mahakamani.”
Mheshimwa Bwege anakula mic “mie leo sichangii mengi. Ninachoona ni kwamba tunaanza kugeuzana mabwege kwa ubwege bwege tu wa mabwege wengine. Haiwezekani mhalifu mmoja alindwe kwa mitutu na mamlaka kaya iwe salama. Tunafanya vitu kana kwamba hatuna ubongo wa kukumbuka historia za waliopita waliowahi kulewa maulaji kiasi cha kujilisha pepo wakaishia kuumbuka. Wako wapi wababe kama Saddam Hussein au Mwamali Kaddafi? Si walipigwa teke na kutokomea wakasahaulika? Hakuna ubwege kama kukinzana na ukweli na mambo yaliyo wazi. Hivyo, mwende Koromije au msiende, haisaidii. Majibu yako hapa hapa kama tutaamua kama jamii ya wachovu wanaochukia na kuchoshwa na ubangaizaji, kubebana na kupatilizana kwa sababu binafsi.”
Sofia Lion aka Kanungaembe anakwanyua mic “siungi mkono wazo la kwenda Koromije. Kwanini mnatka kufukua makaburi ambayo mtashindwa kuyafukia? Kwanini suala hili limepewa uzito kuliko mambo mengine? Kama mmesahau makaburi kama Escrow, EPA, IptL na sasa Symbiosis ambayo juzi ilishinda kesi ya kuibia mabilioni kaya, kwanini msijisahaulishe na hili ili msiumize mioyo yenu? Sioni kama kuna haja ya kuendelea kuwapigia mbuzi gitaa zaidi ya kuacha wakati ufanye kazi yake. Naungana na Mheshimiwa Bwege. Tuache ubwege na mambo ya kibwegebwege kwenye mambo ya umma.”
“Du, da Sofi hapa umefunga nyama na kufumba!”
Kijiwe kikiwa kinapita si akapite Bashiiit! Kama siyo kuzungukwa na ndata na mitutu mbona tungemfanyia kitu mbaya!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.