Quantcast
Channel: Free Thinking
Viewing all articles
Browse latest Browse all 3175

Magufuli atafakari sana vita dhidi ya mihadarati

$
0
0

            Akihutubia bunge la kwanza akiwa rais, Dk John Magufuli aliwaahidi watanzania kupambana na biashara haramu ya mihadarati ambayo imekuwa aibu, kero na tishio kwa taifa. Alisema kuwa hatakuwa na simile na wauza unga na atawasaka vinara wote wa jinai hii. Kwa kazi ambazo ameishafanya na mifano yake, Magufuli anamaanisha asemacho na kusema amaanishacho. Kwani ana mapenzi na mipango ya dhati na kweli kwa watanzania ambao kadhalika wanamuamini na kuwa tayari kushiriki; na kushirikiana naye katika vita hii ya kulikomboa taifa.
            Pamoja na dhamira safi na juhudi kubwa za kupambana na jinai ya mihadarati, rais Magufuli anapaswa kufahamu baadhi ya mambo –kama hajayafahamu na kama anafahamu abadili mkakati kutoka ukalipiaji hadi ukamataji wahusika na kuwafikisha kunakostahili. Rais Magufuli ni msemakweli anayeamini katika uwazi. Sentensi “Msemakweli ni mpenzi wa Mungu” huwa haikauki kinywani mwake. Hata hivyo, mambo mengine –hasa yanayohusiana na usalama –hayahitaji ukweli kuwekwa wazi. Kwani kufanya hivyo kunaweza kumgharimu mhusika. Na huu ni ukweli tu.  Kwa mfano, wauza unga wameonyesha kuwa na uwezo mkubwa kifedha na kimkakati kiasi cha kuyumbisha utawala uliopita kiasi cha kujenga hisia kuwa wakubwa zake walikuwa na namna walivyokuwa wakinufaika na kadhia hii. Kwa kutumia fedha, ushawishi, mitandao na mikakati yao, wauza mihadarati waliweza kuuhujumu na kuuweka mfukoni utawala uliopita ukiachia mbali kuwaua baadhi ya watu walioshupaa kupambana na kadhia hii.
            Jambo la kwanza analopaswa kufanya rais na timu yake ni kupunguza maneno na kuongeza matendo. Achukue mfano wa rais wa Marekani, Barack Obama anavyopambana na ugaidi duniani. Obama huwa hasemi atafanya nini na vipi. Badala yake hutenda na kutangaza baada ya kutenda kama alivyofanya alipofanikiwa kumuua kiongozi wa mtandao wa al-Qaeda Osama bin Laden na vinara wengine waliouawa kwa kutumia ndege za drone kwenye maeneo sugu na mazalia ya ugaidi.obama husema machache na kufanya mengi na hii ndiyo siri ya ufanisi wake katika kupambana na ufisadi.  Hivyo basi, badala ya rais kuapa na kuahidi atapambana na wauza unga, anapaswa kuanza kuwasaka na kuwakamta ndipo atangaze. Anaweza kufanya hivyo hata kwa mafisadi, vidokozi, wala rushwa, wakwepa kodi na wahalifu wengine wanaokwamisha maendeleo ya taifa letu.
            Katika makundi yote ya kihalifu, hakuna kundi hatari na linalotishia usalama wa taifa letu kama magenge ya wafanyabiashara haramu ya mihadarati. Wana fedha, ushawishi, mitandao hata ndani ya serikali kiasi cha kuweza kutumia uwezo huu haramu na hatari kuhatarisha maisha ya yeyote anayetaka kuyaangamiza. Historia ni shahidi. Wako wapi akina Amina Chifupa waliojitolea kufichua uovu huu? Rejea jinsi rais mstaafu Jakaya Kikwete alivyopewa orodha ya wauza unga na wahalifu wengine akashindwa kuzifanyia kazi. Je aliogopa au kuzuiwa na nini? Je kulikuwa na namna alivyokuwa akinufaika na jinai hii au aliogopa hatari iliyoko nyuma ya magenge haya? Hivyo, rais –japo ni taasisi –anapaswa kuzingatia na kuchukua tahadhari dhidi ya kitisho hiki hasa ikizingatiwa kuwa wakubwa wa magenge haya wengine wamo serikalini na kwenye taasisi mbali mbali za binafsi na umma. Hakuna tahadhari na mkakati bora wa kuwazidi kete wahalifu kama kuwakamata kwanza na kutangaza baadaye. Maana unawastukiza na kuwanyima nafasi ya kujihami kwa kuhujumu mikakati yako.  Magenge ya wauza mihadarati ni tishio hili si kwa Tanzania tu bali kwa dunia nzima.  Rejea kugundulika kwa wakubwa wa megenge ya wauza mihadarati wenye nchi ya Guinea Bissau ambapo mkuu wa majeshi aligundulika kuwa kingpin wa jinai hii. Rejea mauaji ya mameya, magavana na viongozi wengi wa juu nchini Brazil pale serikali ilipoamua kupambana na mihadarati. Rais bado anahitaji watendaji waaminifu na walio tayari kumsaidia katika mapambano haya.  Pia awatumie wala na wavuta unga ili kuelekeza vyombo vya upelelezi kwa wale wanaowauzia unga.
            Pamoja na ukweli kuwa rais Magufuli amekuwa serikalini kwa muda mrefu, hivyo, anajua aina ya magenge anayopambana nayo, anapaswa kuchukua tahadhari zaidi. Watanzania wanamkubali na kumpenda na wako tayari kushirikiana naye kukomboa taifa lao toka kwenye kashfa na aibu ya mihadarati, ufisadi, ujambazi, rushwa na uchafu mwingine. Pamoja na kujihami yeye binafsi, anapaswa kuwalinda watoa taarifa, wakamataji na magereza kwa ujumla kwa kuhakikisha wahusika wanapokamatwa hawataroshwi. Muhimu, rais angeaanza kukamata na kutangaza baadaye.
            Tumalizie kwa kumsisitiza rais umuhimu wa ukimya katika kuwasaka vinara wa biashara haramu ya mihadarati. Kamata kwanza, tangaza baadaye. Pia chukua hatua za haraka kuhakikisha vinara wa mihadarati wako magerezani na si uraiani wakipanga kuhujumu juhudi zako hata kukuangamiza. Kwa leo tunaishia hapa.
Chanzo: Tanzania Daima Januari 17, 2016.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 3175