Quantcast
Channel: Free Thinking
Viewing all articles
Browse latest Browse all 3173

Mlevi akataa tuzo kanyabwoya ya mlevi bora

$
0
0

           Kuna kijigazeti cha kitapeli kiitwacho Afro Jua Times kilitaka kuniingiza mjini na kunitumia kikidhani mimi ni njinga na mpenda kusifiwa ujinga kama wale wanaopenda kila upuuzi ilmradi wamesifiwa hata kwa ujinga.
            Kijigazeti hiki –ambacho bila shaka kinamilkiwa na matapeli wa kibongo na kinigeria eti kilinitangaza kama mlevi wa mwaka wakati hakuna nilichowafanyia walevi zaidi ya kushirikiana na wezi kuiba kanywaji kao. Eti kilitaka niende kupokea tuzo hii kichaa utadhani mimi kichaa au Njaa! Hata hivyo –hata ingekuwa kweli nimefanya mambo makubwa kwa walevi –nani anapaswa kujua ubora wa mlevi kati ya walevi na hawa matapeli wa ulaya? Nimewastukia hawa matapeli uchwara wanaotaka kunitumia niwapigie ndogo ndogo kwa Dk Kanywaji baada ya kugundua kuwa tulisoma wote na ni swahiba yangu mkubwa. Nasema wazi mmenoa na mkome na kukomaa. Bongo siyo shamba la bibi tena tangu rafiki yangu Dk Kanywaji akamate ukanda.
            Historia hii ya matapeli kutaka kunigeuza mumu au mpumbavu kwa lugha ya matapeli wa kinegeria inaanzia mbali. Kuna kipindi nilipewa shahada feki ya Udaktari na chuo kimoja cha mtaani kule majuu baada ya kugundua mimi ni kihiyo na mpenda sifa. Punde si punde nikapewa tuzo na wachunaji uchwara na baadhi ya NGOs. Kwa vile walinipata kabla sijawabamba kuwa ni matapeli, waliona mimi ni mumu ambaye wanaweza kumtumia watakavyo. Kama ni kuwa mumu basi wao ndiyo mumu ila siyo mlevi kama mimi bonge la mjanja ambaye nimepiga vitabu kuliko hata ninavopiga ulabu. Guess what. Nimepiga shule hadi nikafikia kibao kisemacho, il n’y a pas plus de classe pour vous. Yaani kwa kisambaa hakuna darasa hapa ndiyo mwisho.
            Kwa wanaotujua wasomi kama sisi na Dk Kanywaji, huwa hatupendi sifa za dezo hasa za kisomi au utendaji. Unakwenda shule haki la mlevi anaona. Unachapa mzigo hadi kila mvivu na mwizi anaona na kupigwa na butwaa. Kwanza, hawa matapeli wamepoteza muda wao. Mimi –sawa na Dk Kanywaji –si watu wa kutumia njuluku za walevi kwenda kuzurura ughaibuni. Si washamba wala malimbukeni wala watu wenye roho mbaya wanaojifanya kutoona jinsi walevi walivyopigika. Hata kama tuzo yenyewe ingekuwa ya ukweli nisingeunguza dola kwenda kupokea upuuzi. Kwa vile mimi ni fyatu, nilipopigiwa simu kuwa nimepata tuzo hii mavi niliamua kuwaambia –kama tuzo ni dili –wawape mama zao waliozaa na kulea matapeli wasiopenda kufanya kazi bali kutapeli wenzao. Walidhani mimi ni bongolala au Vasco da Gama mpenda kuzurura hata kwa vitu vya hovyo? Thubutu yao. Hawampati mtu hata kwa chembe.
            Kama ninastahiki tuzo, basi, tuzo hiyo nitapewa na walevi ambao napanga kuacha kuwabia na kuwatumikia kama Dk Kanywaji anavyotumikia wachovu wa kaya hii iliyokuwa imenajisiwa na vihiyo, mafisi, mafisadi, malimbuke, wavivu, wazururaji, wasanii na wajinga waliokuwa wakitumia masaburi kufikiri badala ya vichwa. Haya ya matapeli na matapeli watapeliwa wenzao tuyaache.
            By the way, ngoja niwape ishu bab kubwa ambayo itanitoa kiasi cha kugeuka bilionea na kuandikwa kwenye gazeti la Forbes. Guess what. Ninataka kuanza bishara ya kuingiza kayani mafuta machafu na kuwalangua wachovu. Maana siku zote sikujua kuwa kumbe wese feki lilikuwa dili na washenzi walikuwa wakiukata wakati sisi tunakatwa na umaskini, ukwete na ukapa! Kwa vile nimeinyaka. Lazima nianze kupiga dili ili nami niwe tajiri ati. Pia nataka kuanza biashara ya kulima miraa. Wasioinyaka misamiati yangu ni kwamba miraa ni mirungi ambayo kule kaya ya jirani ambako binadamu waliamua kujigeuza mbuzi wakibugia majani kama hawana akili nzuri miraa ni dili bab kubwa. Nimeishapata eneo kule upareni ambako nitalima hii kitu na kuula kama wengine.
            Wakati nikingoja wafanyakazi wamalize kulima hii kitu na kuvuna –kwa vile nimesoma ma-commerce, business na madude mengine ya kitapeli lazima nibadili jina na kujiita Mpayukaji Kanywaji ili niweze kuomba kazi pale Banki kuu sawa na vitegemezi vingine vya wanene vilivyojazana pale ambavyo Dk Kanywaji naona hajavistukia na kuvitumbua hata kama ni vijipu vilivyozaliwa na mabusha ambayo nayo hajayatumbua. Hii ikibuma basi nitaamua kufanya kitu kingine ambacho kitaishangaza dunia. Guess what.  Hebu soma taratibu, nitaanza kukusanya habari za Dk Kanywaji nijue kama ana kabinti ambako hakajaolewa nikaoe ili nami niwe mkwe wa dingi ili anikumbuke. Jamaa anavyopenda wachovu na wanyonge, najua atafurahi kusikia kuwa Ayatollah Mlevi ameamua kuwa mkwewe ili nibadili jina vizuri.
            Wakati nikisukuti jinsi ya kutoka, ngoja niende kwa mama Ndiza nikapate kanywaji halafu niende mitaa ya Lumumba kununua kete mbili hivi za bwimbwi nibembee kwenye maraha yangu nikiota kuwa bahari tena wa nchi kavu.
Chanzo: Nipashe Januari 16, 2016.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 3173