Rais Jakaya Kikwete ni mtu asiyeishiwa vituko. Wakati mwingine akiongea –licha ya kujipinga hata kujipiga kijembe –wenye kuchambua mambo hushangaa kama anasoma hizo hotuba anazoandaliwa kabla au kusema baadhi ya mambo akiwa anajua uhalisia wake. Maana mambo mwengine anayosema yanamsuta na kumuacha akionekana tatanishi kwa umma unaoyapokea. Hivi karibuni Kikwete aliwaacha wengi hoi aliposema, “Kazi niliyoamua kufanya sasa na baada ya kuacha urais ni kusaidia uhifadhi.” Kwanini baada ya kustaafu na si wakati akiwa madarakani? Nadhani kama rais alikuwa na nia njema na mali na raslimali za taifa wakiwamo wanyama, angetumia rungu lake kama rais kupambana na ujangili ambao unatishia kufuta baadhi ya wanyama wetu kwenye ramani ya nchi na ya dunia.
Vituko na maneno ya Kikwete yanatukumbusha aliposema kuwa wanafunzi wa kike wanaopoachikwa mimba na vishoka ambao hawashughulikiwi wanaponzwa na kiherehere chao wakati umaskini na ufisadi uliotengenezwa na watawala kama yeye una mchango mkubwa pamoja na sababu nyingine. Je halijui hili au hajajulishwa? Je alionaje kuwa ni kiherehere tu na si umaskini, ugumu wa maisha, ukosefu wa huduma kama vile usafiri kwa wanafunzi, walimu wa kutosha na kutamalaki kwa rushwa ya ngono pamoja na mambo mengine? Je hivyo navyo ni kiherehere au waliovisababisha nao wana kiherehere?
Kikwete aliahidi kutumia muda wake wa ustaafu kuwatunza mbwamwitu. Wengi walidhani –kwa vile wanyama kama Tembo na Faru ndiyo wanakaribia kumalizwa –lau angeanza na hawa ingawa nalo laweza kuwa siasa tu majukwaani kutokana na ukweli kuwa hakuwalinda vilivyo wanyama hawa wakati akiwa madarakani sawa na alivyofanya kwa vitu vingine kama mikataba ya uwekezaji aliyoahidi angeiweka wazi na kuifumua na kuisuka upya asifanye hivyo. Hata hivyo, wanaomfahamu Kikwete kama mtu mwenye kupenda kusema maneno mengi ya kufurahisha na kutoa ahadi kemkem asitekeleze hata moja hawamchukulii seriously. Yako wapi maisha bora kwa wote aliyoahidi akiingia madarakani au nayo atayashughulikia baada ya kustaafu? Inashangaza mantiki ya Kikwete kuona mbwamwitu ndiyo wa kutunzwa wakati tishio la kutoweka kwao wala thamani yao havilingani na la twinga na faru. Ni ajabu kuwa na uchungu na mbwamwitu ukaachia wanyama walio kwenye hatari ya kutoweka kama tajwa hapo juu watoweke.
Kama wanyamapori wameteketezwa hadi kuuzwa nje wakiwa hai na hakufanya lolote atajitosa kufanya nini na kwanini sasa baada ya wanyama wenyewe kutishia kutoweka? Ina maana Kikwete amesahau mkasa uliotokea chini ya uangalizi wake na asichukue hatua hapo Novemba 26, 2010 ambapo wanyama wapatao 150 wakiwamo twiga hai walisafirishiwa kwa dege la kijeshi kwenda Qatar? Je alifunga wangapi ukiachia mbali serikali yake kujenga mazingira yaliyomwezesha mtuhumiwa toka Pakistan kutoroka kwa hofu ya kuwaumbua wakubwa waliokuwa nyuma ya ufisadi huu wa kishenzi na kutisha? Kwa mtu mwenye uchungu na raslimali za nchi tukio kama hili lingeonyesha uchungu na ukali wake dhidi ya jinai hii, lakini wapi. Kwanini kufanya hivyo baada ya kustaafu ambapo hatakuwa na madaraka na kushindwa kuwatunza alipokuwa na madaraka?
Kikwete alikaririwa akisema, “Ni aibu wanyama hawa muhimu kwa utalii kutoweka kisha baadaye tuwatafute kwa gharama kubwa… Mimi niko tayari kusaidia wanyama hawa wasipotee.” Je hao wanyama waliosafirishwa kwenda Qatar wakiwa hai hapo mnamo tarehe hawakuwa wanyama? Kama ni aibu basi mwenye kuistahili na aliyeilete si mwingine ni Kikwete ambaye serikali yake ilishiriki kikamilifu kuwatorosha wanyama huku katibu wa wizara wa wakati ule aliyetuhumiwa moja kwa moja kusuka na kutekeleza uhujumu huu akiteuliwa balozi kwenye nchi moja jirani. Kama Kikwete ana uchungu na wanyama kama anavyotaka aonekane, ilikuwaje akampandisha cheo mtu mwenye kushutumiwa ambaye ukiachia hilo alipaswa amwajibishwe kwa sababu wizara yake ilishindwa majukumu yake kiasi cha kuruhusu wanyama hai wasafirishwe tena kupitia kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Je serikali ya Kikwete inaweza kukwepa lawama kwa hili iwapo hata walinzi wa uwanja wa ndege hawakuwa na uwezo wa kuzuia hao wanyama kutosafirishwa kwa vile ulikuwa ni mzigo wa wakubwa? Je hapa Kikwete ana tofauti na rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye chini ya utawala wake mbuga maarufu ya Loliondo iliuzwa kwa waarabu hao hao kutoka Ghuba? Je huku si kukumbuka blanketi asubuhi kama siyo porojo za kisiasa?
Tumalizie kwa kumshauri Kikwete aache kututia vidole machoni na kutudhihaki kuwa atatunza wanyama wakati serikali yake ilihalalisha ujangili kiasi cha kutisha.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 20, 2015.