Hivi karibuni watanzania walishuhudia mashindano ya kuonyesha ukwasi na “upendo” wa wanaopigiwa upata kutoa mgombea wa chama tawala CCM. Mafahari wa tatu kati ya wengine wanaopigiwa upata kuutaka urais kupitia CCM, Mizengo Pinda waziri mkuu wa sasa, Bernard Membe waziri wa mbo ya nchi za nje na Edward Lowassa waziri kuu aliyetimliwa na kashfa ya Richmond walikutana Zanzibar na kuonyesha utajiri wao wakati wa hafla ya kuchangia mfuko wa maendeleo wa mkoa mpya wa CCM wa Magharibi huko Zanzibar
Hata hivyo, wengi wanashangaa jamaa walivyopata huu utajiri ambao si wa kawaida kwa viwango vya kitanzania ukiachia huu moyo wa kutoa. Kwanini wawe na upendo na moyo wa kutoa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu kama siyo hongo kwa chama ili kiwapitishe? Na kwanini CCM haiwatakishi maelezo ya jinsi walivyochuma huu utajiri? Kweli CCM hii inayopokea na kushabikia fedha zenye kila dalili ya shaka inaweza kuongoza mapambano dhidi ya ufisadi na rushwa? Je watu wenye jeuri ya fedha hii wanatumia, kuweka benki, kuwekeza kiasi gani? Je wana wafadhili wasiotaka kujulikana walioificha nyuma ya “marafiki” wanaowatumia kulinda maslahi yao ya kibiashara au kifedha? Swali muhimu na kubwa linalowasumbua wengi ni uhalali wa fedha husika. Je kama kwenye tukio dogo na moja kama hili wanatoa mamilioni kiasi hiki, kwenye uchaguzi watamwaga mabilioni kiasi gani ili wayarejesheje bila kuiuza nchi? Je tunahitaji rais mwenye jeuri ya fedha au mwenye uchungu na maisha ya wenzake? Nadhani wakati wa wagombea kutaja vyanzo na ukubwa wa utajiri wao umefika ili kuepuka kuendelea kuweka wezi, mafisadi na wasaka tonge ikulu ili waendelee kuichezea na kuiuza nchi yetu.
Vyombo habari viliripoti kuwa Pinda na marafiki zake kuchangia jumla ya Sh203 milioni. Huku Lowassa, Membe na marafiki zao walichangia jumla ya Sh101.5 milioni. Wengi wanaendelea kushangaa utajiri wa hawa jamaa ambao wanaweza kuunguza mamilioni ya shilingi huku wakijua wazi kuwa atateuliwa mtu mmoja tu kati ya wote wanaotaka kugombea urais. Kimsingi, wanachofanya ni kama kununua tiketi ya bahati nasibu kwa mamilioni bila kuchelea kukosa. Mtu wa namna hii lazima atakuwa na ukwasi si wa kawaida. Je ameupataje? Je hawa wanaotwa marafiki wa vigogo hawa wakisiasa ni akina nani? Wahusika hawataki kutaja wala kuweka mambo wazi.
Wamefanya vizuri kuuonyesha umma wa watanzania ni mafisadi kiasi gani hawa walivyo. Haya mamilioni wanayochanga bila shaka waliyaiba toka kwa watanzania kama siyo kuhongwa wakifanya kazi ya watanzania. Hawafai. Nadhani huu ni ushahidi kuwa kwa sasa CCM haina tena aliye msafi wala mwenye kufaa kuongoza nchi kama tutakuwa wakweli kwa nafsi zetu.
Kwa vile msimu wa kugeuzana mabunga na wasahaulifu umewadia, watanzania wategee vimbwanga kibao ambapo pesa chafu itokanayo na rushwa, mihadarati na ujambazi mwingine itaingizwa kwenye mzunguko kwa njia ya takrima kama hizi tunazoongelea. Wasafishaji hawa wa fedha haramu ima wao au mawakala na wafadhili wao watatumia fursa hii kusafisha fedha yao chafu huku wakijenga mazingira ya kujiweka karibu na watakaopitishwa na kushinda uchaguzi tayari kwa kutengeneza fedha zaidi.
Wanaodhani huu ni uzushi wajiulize swali moja kuu: Kwanini sarafu ya Tanzania huporomoka sana kila unapokaribia na baada ya uchaguzi? Jibu ni simpo. Watawala huamuru ichapishwe fedha nyingi na kuingizwa kwenye mzunguko kinyemela kiasi cha thamani ya shilingi kuporomoka kama inaharisha kama ilivyo sasa. Kwa ushauri tu, wanaotaka kununua au kuuza mali wafanye hivyo kwa sasa. Maana baada ya uchaguzi shilingi itakuwa hoi. Kwa anayetaka kuona mkururo (trajectory) ya sarafu ya Tanzania na namna ambayo imekuwa ikishuka, aangalie thamani yake kila unapokaribia uchaguzi. Angalieni kuanzia 1985 alipong’atuka Mwalimu Julius Nyerere, 1990, 1995, 2000, 2005 , 2010 na sasa 2015 mtakuta kuwa kila baada ya miaka mitano ima karibu au baada ya uchaguzi sarafu yetu huporomoka ikilinganishwa na dola ya kimarekani.
Hawa wanaomwaga mamilioni ukiwauliza wameyapata wapi hawatakupa jibu. Wapo wanaosema kuwa mishahara yao ya ubunge inawatosha kutoa kiasi kikubwa kama hiki. Si kweli. Kwa watu wanaopenda kupata kuliko kutoa, kama si uchaguzi kuwalazimisha wasingefanya hivyo. Kimsingi, ni kwamba watawala wetu hawako tayari kugusa fedha yao zaidi ya kutaka iongezeke. Hapa tunachoweza kusema ni kwamba wapo watu wachafu hasa wafanya biashara iwe halali au haramu wameishawanunua watu wao ambao nao sasa wanataka kuwanunua watanzania. Kusema eti wanatoa mifukoni mwao hili haliingii akilini. Kama watu wako tayari kutumia magari ya umma huku yao wakiyafungia nyumbani, sijui kama watu wa namna hii wanaweza kutoa hata senti kwenye fedha itokanayo na mishahara yao vinginevyo mishahara yenyewe iwe ile fichi.
Tumalizie kwa kuwataka watanzania hasa wapiga kura kula fedha ya hawa wanaojionyesha wanazo na kisha wasiwapigie kura. Maana wakiwapigia kura watakuwa wamewapa fursa ya kuwauza na kurejesha fedha wanayowahonga sasa maradufu huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa umaskini na ukosefu wa huduma bora zaidi zaidi kwa miaka mitano ijayo. Kama watoa fedha chafu hawa wanavyowageuza majuha kwa kutaka kuwatapeli, basi kuleni fedha yao lakini kura yenu msiwape ili wengi wafe kwa ugonjwa wa moyo baada ya uchaguzi.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 13, 2015.