Quantcast
Channel: Free Thinking
Viewing all articles
Browse latest Browse all 3175

Mlevi anusurika kufa kwa madawa ya kichina

$
0
0
  • Chinese-herbalist-008.jpg
          Baada ya kaya yetu kuhalalisha haramu ya sera holela chini ya kisingizio cha ruksa na biashara huria si matapeli wengi waliingia kayani kiasi cha kuhatarisha maisha ya walevi. Hata bangi tunayovuta na ulabu tunaopiga mwingine unaagizwa toka nje utadhani hatuna zana hizi.
Juzi si ngiri ikapanda. Kwa vile mahospitali yalikufa zamani yakabaki kuwa vyanzo vya madawa kwa famasi zinazomilkiwa na madaktari na wafanyakazi wengine wa hospitali za umma, niliamua kwenda kwa mchina kupata dawa.  Niliamua kwenda kwenye tiba mbadala hasa kwa kuogopa kwenda hospitali nikatolewa upepo wa kuomuona daktari utadhani ni kidosho mzuri mzuri. Mie si mshamba kiasi hicho kuibiwa mchana wakati ni njanja. You know what. Mganga niliyemwendea si mchina. Mganga mwenyewe hata Kiswahili hakimanyi ukiachia mbali kuonyesha wazi alivyo msanii zaidi ya tabibu. Hata hivyo simlaumu hasa ikizingatiwa kuwa hii kaya ni ya wasanii watupu kuanzia wazito hadi wepesi. Hamuoni wanavyofanya usanii wao kwenye kila jambo hadi hata kwenye elimu? Hayo tuyaache.
Alinipa dawa zenye maandishi ya kichina huku akijitahidi kunifafanulia kwa kichina. Maranǐhǎo,hǎo jiǔ bú jiàn wǒ hěn hǎo, hiinnhoo, huuunhiii, heeiieye, guo feng hua nung kong huuunhaaniii kom. Mswahili na kichina wapi na wapi? Basi shida mwanaharamu. Kwa vile lisirikali lilishanitoa kafara ilibidi nipwakie hii midawa ya kichina. Kufika nyumbani, bi mkubwa akanichemshia maji na kuchanganya na kunipa ninywe. Punde si punde si nikasikia sauti za radi na ngurumo tumboni mwangu. Wacha niendesha hadi nidhani nitanonihino utumbo!
Baada ya kukutwa na ya kunikuta nilijiuliza maswali bila majibu. Je inakuwaje hawa wajalaana wanawaruhusu wajalaana wa kichina kuja kutupa midawa ambayo hata maelezo yake hatujui? Je ni ufisadi na ujinga wa wanene wetu? Bila shaka hapa kuna mtu amehongwa kitu kitu ili hawa matapeli waje kufanya biashara yao. Kwanza siamini kama biashara wanayofanya ni ya hii midawa ya kufanya mtu aendeshe kama mkangafu. Huenda kuna biashara nyingine hasa ikizingatiwa kuwa kaya yetu ina tembo na faru wengi. Hayo tuyaache. Kama twiga wanauzwa hai tena mchana, kwanini wajamaa wasifanye vitu vyao? Waduwanzi ndio waliwao au vipi?
Hebu tuzidi kujiuliza hata kama ni kibangi bangi na mma mma. Je mswahili anaweza kuuza miti shamba yake uchina asizuiliwe au hata kubaguliwa kama jamaa zangu wa dukani ya Huarang pale Ursino street? Sijui nao hii kesi yao ya racism-cum-apartheid-cum –dihumanization imeishia wapi?  Je tunawaamini vipi hawa watu tena ambao baadhi yao wanatubagua wazi wazi?
Baada ya kujiuliza maswali haya, niliamua kwenda kwenye maktaba yangu kujisomea lau nipate majibu kama siyo maelezo ya kutosha. Katika pitapita yangu si nikapata kitabu cha mzee Mchonga cha Freedom and Development na Crusader for Liberation. Kusema ukweli nilisoma na kupata mengi hasa juu ya dhana nzima ya kujikomboa kiakili yaani Mental emancipation. Nilichojifunza toka kwa gwiji huyu (Mwenyezi Mungu ameneemeshe na kumpuzisha) ni kwamba tunatawaliwa kijinga kwa sababu sisi ni wajinga. Dawa ya moto ni moto. Ukiwa mjinga unatawaliwa kijinga na wajinga huku kila kitu kikifanyika kijingajinga nawe kwa ujinga wako hutafuti suluhu ya kuondokana na utawala na mambo ya kijinga jinga kwa vile u mjingajinga.
Ili kujitoa katika ujinga niliuliza maswali mengine makali. Je afrika imeishiwa miti ya kutibia madawa ya kiafrika? Je ni wachina wangapi wako tayari au wanatibiwa kwa miti ya kiafrika tena na waganga wa kiafrika? Thubutu! Ukipatwa na kiherehere ukaenda kule na mitunguli yako wanakurambisha shaba wakisema ulikuwa umebeba bwimbwi. Je kabla ya kuja wachina mababu zetu walijitibia na nini? Au ni kwa vile wanene wanakwenda zao kutibiwa India huku wakiacha wachovu wapukutike kama inzi? Kama mitishamba ya kichina ni bab kubwa kwanini wanene wetu wanatibiwa India badala ya uchina? Hapa kunani kama siyo gea ya kutuingizia wakimbizi wa kiuchumi waliotamalaki mitaani wakichoma mahindi na mishikaki huku tukiaminishwa ni wawekezaji wakati ni wachukuaji wa ajira zetu na wakimbizi wa kiuchumi tena wenye kufanya biashara haramu kama vile pembe za ndovu na madanguro kama hawa wa Huarang?
Najua jamaa zangu wa Huarang watakana kuwa si wabaguzi wa rangi kama wenzao wa kigabacholi. Basi kuwaumbua nitapendekeza nimuoe yule kidosho wa Huarang anayesemekana kuwafokea waandishi wa habari waliotaka kujua ni kwanini anabagua waswahili. Loooh! Nimechemsha! You know what. Kutokana na kupiga mibangi nimeanzia stori katikati. Ni kwamba hivi karibuni kule kwenye mtaa wa Ursino kwa wanene, waandishi wa umbea waligundua duka moja la kuuza makulaji ya kichina liitwalo Huarang ambalo haliruhusu weusi kungia mle. Kwa hiyo ukiona Huarang ujue ni makaburu wa kichina waliopo hapa kayani wakilindwa na mafisi na mafisadi wanaonufaika na biashara hii ya dangulo.
Guess what. Wabaguzi wa rangi wana tabia zinazofanana. Hata magabacholi wamekuwa wakiendesha madangulo kwa kisingizio cha kuleta vidosho toka Bombei kuja eti kucheza Bhangra na Mujra. Urongo. Yote hayo ni mandangulo ambapo kwa ubaguzi wao hata madhambi wanafanya kibaguzi.
Kama kaya yetu isingekuwa ya wajinga wajinga ikiliwa na kutawaliwa kijinga jinga huyu jamaa ningemuondolea uvivu nikamshitaki anilipe fidia kwa kupunguz kitambu changu tokana na kuendesha. Pia ningedai fidia kwa maumivu aliyonisababishia ukiachia mbali presha ya kunyotoka roho. Maana alinilisha sumu tena kwa kuniuzia.
Hivyo, ndugu zanguni, ndivyo nilivyonusurika kufa kwa midawa ya kichina. Je ni wangapi wanaonyotoka roho tokana na mchezo huu bila kuongeza wanyama zetu hasa wale wenye vipusa na pembe? Hapa sijagusia ubaguzi wa akina Huarang.
Chanzo: Nipashe Mei 9, 2015.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 3175