Si uchochezi kusema kuwa watawala wetu wameshindwa, tena vibaya sana. Ni aibu kwa taifa ambalo limesherehekea miaka 53 ya uhuru kushindwa kufanya maamuzi magumu hadi lishinikizwe na wafadhili. Tishio na amri ya hivi karibuni toka kwa serikali ya Marekani kwa Tanzania kuwa haitatoa fedha za Changamoto za Milenia (MCC) kama serikali haitawachukulia hatua watuhumiwa wa kashfa ya uchotaji wa mabilioni ya fedha za umma, escrow ni somo tosha.
Heri wafadhili wamenena. Hili ni pigo na aibu kwa rais Jakaya Kikwete, serikali na CCM ambao wamekuwa wakiwahadaa watanzania kuwa wako madarakani kwa maslahi yao wakati hali ni tofauti. Huu ni ushahidi kuwa CCM na serikali yake wamewekwa mfukoni na mafisadi. Hali ikiendelea hivi, watawala wetu wataipeleka nchi kubaya. Huu ni ushahidi tosha kuwa utawala wa sasa umechoka, upumzishwe ili wenye uwezo watawale na kusafisha uchafu uliopo. Inakuwaje wananchi wanashindwa kuona haya na kuiwajibisha vilivyo CCM kwa kuishikisha adabu?
Ni ajabu kwa nchi inayojidai kuwa na utawala wa sheria lakini ikawekwa mifukono mwa matapeli wachache, wasaka tonge na wahalifu wa kawaida. Ziko wapi tambo za kupambana na biashara ya madawa ya kulevya? Nani anawagusa? Je hawa hawana ubia kwenye serikali ya sasa? Je hawa hawajaiweka serikali mfukoni? Asitokee mtu akaniambia kuwa hawajulikani. Mbona rais alishakiri kupewa orodha ya wauza unga asiifanyie kazi kwa sababu ajuazo? Je inakuwaje tunashindwa kupambana na ufisadi ilhali tukijua kuwa ni kikwazo kwa maendeleo ya taifa? Je ni kwa vile mafisadi ni washirika wa nyuma ya pazia ya watawala wetu?
Najua wengi wanaweza kusema tunaizushia serikali. Kama watachunguza sababu za serikali kuruhusu ufisadi kuwa sehemu ya maisha ya serikali yetu, wataelewa tunachosema. Hivi kweli nchi inayoamriwa na wafadhili la kufanya ni huru? Je kwa uzembe na upofu wetu tunapaswa kuwalaumu wafadhili kwa kuingilia mambo yetu? Watashindwaje kuingilia iwapo tunafanya mambo ya kitoto na ya hovyo? Imefikia mahali hata bunge linatoa maagizo halafu wakubwa wanayadharau na kuja na mambo yasiyo ingia kichwani kama ilivyotokea juzi wakati Ikulu iliposema kuwa haitawawajibisha watuhumiwa wa wizi wa escrow wala kuchukua hatua hadi ifanye uchunguzi wake. Tambo za ikulu zimeishia wapi baada ya kubanwa? Ndani ya wiki moja ikulu, ikiwa imechanganyikiwa na kujichanganya ilitoa tamko jingine la kijichanganya zaidi ikisema kuwa rais atawashughulikia watuhumiwa ndani ya wiki moja. Hii maana yake ni kwamba ikulu imeminywa na kufanya kile ambacho haikutaka kufanya. Maana ukiangalia timing ya tamko la Marekani na mkengeuko wa Ikulu unagundua kuwa hata kama rais atawawajibisha wahusika si kwa kutaka bali kulazimishwa na wafadhili. Je rais au chama kinachounda serikali vya namna hii bado vinawafaa watanzania? Je ni vibaya kusema kuwa rais amegeuka mhimili wa ufisadi anaopaswa kuuchikia na kupamba nao? Je ni kwanini inakuwa hivi kama rais hanufaiki na jinai hii au kuishiriki?
Ushahidi wa kimazingira unaonyesha wazi kuwa, kama si papara za bunge, au tuseme kuwekwa sawa na kuingia mkenge, lilipaswa kuiwajibisha serikali yote. Kwa vile inaonyesha escrow ni dili lao. Haiwezekani mawaziri tena waandamizi na maafisa wengi wa serikali waruhusu wizi wa mabilioni hivi kusiwe na mkono wa wakubwa zao. Nani anakanusha kutajwa kwa afisa wa ikulu Prosper Mbena anayedaiwa na kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwa aliandika barua ya kushinikiza pesa zichotwe? Je hapa tunatafuta ushahidi upi wa kuihusisha ikulu? Ushahidi mwingine ni ukimya wa muda mrefu wa serikali. Hata kitendo cha rais kusuasua hadi alazimishwe na wafadhili kuchukua hatua ni ushahidi tosha ukiachia mbali rais kuhusishwa moja kwa moja na uletaji wa kampuni jizi ya IPTL hapo mwaka 2004.
Laiti wafadhili wangekwenda mbele zaidi na kuhakikisha hili jinni linalotunyonya damu IPTL linafurushwa na wahusika kufungwa, wangekuwa wametukomboa hata kama wakubwa watalalamika kuwa wanaingiliwa. Kwanini wasiingiliwe iwapo wamejirahisi kiasi cha kuacha mafisadi wajifanyie watakavyo? Kwanini wasiingiliwe iwapo wameonyesha wazi walivyo wa hovyo na fisadi? Nani angeweza kumwamrisha baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere katika lolote? Je ilikuwaje Nyerere akaogopewa na kutopewa amri? Jibu ni rahisi. Alikuwa msafi na mwenye visheni tofauti na hawa walioigeuza ikulu deni la wezi kama alivyowahi kuonya Nyerere huku akiwakataa wengi wa tunaowaona leo madarakani wakiyafuja ili kutimiza utabiri na madai ya nguli huyu (Mungu amlaze pahali pema peponi). Rais anayeamrishwa kufanya alichoapa kufanya amebaki na nini? Je nafsi zo zinawasuta? Je sisi tunawasuta na kuwawajibisha au kuendelea kuwagwaya?
Tumalizie kwa kuwataka watanzania kutorudia makosa. Kwenye uchaguzi ujao licha ya kuhoji ni kwanini ufisadi uliachiwa kuwa sehemu ya utawala wasiangalie sura wala ukongwe wa chama. Wahakikishe wanajipatia serikali safi, mpya, yenye mapya na si huu wendawazimu wa siku zetu. Maana waingereza husema “insanity is doing the same thing over and over again and expecting different results.” Tuachane na wendawazimu huku tukijitofautisha na mafisadi ili mataifa mengine yasiendelee kutucheka kwa kuruhusu taifa letu kuwa shamba la bibi tena bibi mwenyewe hamnazo. Imetosha, wananchi wanapaswa kuanza kwajibika kwa kuwawajibishwa watawala fisadi na wachovu na wabovu.
Chanzo: Tanzania Daima leo.