
Taarifa tulizo nazo ni kwamba mwana wa mfalme wa Danganyika, Ridhiwan Kikwete "alishinda" kura za maoni katika chama cha baba yake Mfalme. Matokeo ya mnyukano wa kugombea nafasi ya atakayepeperusha bendera ya Chama Cha Marithishano (CCM) yanasomeka kama ifuatavyo:
Prince Ridhiwan Kikwete kura 758
Shebby Iman Madega kura 335
Othman Ramadhani Maneno kura 206
Changwa Mohamed Mkwazu kura 12
Jumla ya kura halali ilikuwa ni 1363 na kura 5 ziliharibika.
Japo ni haki ya kila mtanzania kugombea cheo chochote, kuja kwa mwana wa mfalme ambaye ametajwa kwenye skandali nyingi za ulaji kuna mgongano wa kimaslahi.
Kama ilivyotokea Arumeru Mashariki, Kalenga, Bumbuli,Kwahani na kwingineko ambako vigogo wameweka watoto wao ili wawatawale watu wao, Chalinze pia imefanya hivyo hivyo. Kesho utasikia first lady akigombea kabla ya shemeji yake yaani kaka yake mfalme kugombea. Huu ni uroho wa aina yake na ni upuuzi kutumia demokrasia kwa vigogo kurithisha madaraka kwa watoto wao. Ukiachia jina Kikwete Ridhiwan ana nini cha mno kufaa kuliko magwiji kama Iman Madega? Ana tofauti gani na wana wafalme wenzake kama vile Hussein Mwinyi, Adam Malima, Januari Makamba, Emanuel Nchimbi, Vita na Zainab Kawawa,Violet Mzindakaya, Godfrey Mgimwa, Sioi Sumari na wengine waliofichwa kwenye sehemu nyingine za ulaji? Je Mwalimu Julius Nyerere angekuwa kipofu na mchoyo hivi akina Ali Hassan Mwinyi na Kikwete ambao wameonyesha upogo wa kuwarithisha watoto wao madaraka wangekanyaga hata ikulu? Mkapa pamoja na udhaifu wake angalau kwenye hili hayumo japo ana mchango katika kurutubisha ufalme huu uchwara. Ni aibu na machukizo hakuna mfano kushuhudia wanyonge wakizidi kuandaliwa viongozi watokanao na koo. Huu, hakina, nao, ni ufalme wa mlango wa nyuma. Je watanzania wataendelea kuubariki na kupigia mhuri ufalme huu wa kifisadi kwa kuupa kura ili ule au wataukataa na kuukatisha? Ni bahati mbaya sana. Tofauti na Kalenga, watu wa Chalinze hawana ubavu. Lazima mwana wa mfalme ashinde hata kama ikibidi kuchakachua.