
Baada ya rais Jakaya Kikwete kuwafuta kazi mawaziri wanne kwa kosa la kutowajibika kwenye wizara zao, umefika wakati wa kumwambia naye awajibike. Sababu za kufanya hivyo ziko wazi. Kama mawaziri walifutwa kwa vile watu wa chini yao walifanya madudu, basi na Pinda na Kikwete wawajibike kwa vile hawa mawaziri walikuwa chini yao. Pinda alinukuliwa akisema,“Waheshimiwa wote wanne wamekubali kujiuzulu na kilichofanya walikubali kufanya hivyo ni kwamba vyombo vilivyohusika viko chini ya usimamizi wao.” Nadhani Pinda ametoa jibu la ni kwanini Kikwete naye wawajibike. Kwani uwajibikaji wa pamoja (collective accountability) unawahusu mawaziri tu.
Hata bunge lingeondolewa kwa vile nao wako pale kufanya biashara ya mapenzi kama alivyonakiliwa mmoja wao akisema kabla ya kulazimishwa kufuta kauli yake ili kukwepa aibu zaidi. Kimsingi, Tanzania haina serikali wala bunge bali genge la wahuni na walaji tu. Hivyo wananchi tungesimama pamoja na kuhakikisha tunatoa somo kwa kuwawajibisha wote.
Nangojea kusikia atakachosema Kikwete kuhusiana na mawaziri mizigo ambao ni hovyo kuliko hata hawa waliotimuliwa hasa Balozi Hamis Kagasheki ambaye ameondoka tokana na kugusa maslahi ya wakubwa.