Quantcast
Channel: Free Thinking
Viewing all articles
Browse latest Browse all 3173

Hongera Kikwete, Tanzania isichezewe

$
0
0
Kagame akifafanua jambo
KUNA usemi wa Kiingereza usemao, ‘extraordinary problems need extraordinary solution’. Hii imethibitika juzi pale Rais Jakaya Kikwete alipoamua kuwatolea uvivu wanaoota ndoto mbaya mchana kuwa nchi yetu ni kichwa cha mwendawazimu.
Ndiyo. Tunaweza kuwa kichwa cha mwendawazimu kwenye ufisadi, elimu, uchumi na uwajibikaji lakini si katika ulinzi na usalama wa nchi yetu.
Ingawa Rais Kikwete ametoa tamko la kuwakaripia wapuuzi wachache wanaodhani wanaweza kututisha na tukaufyata, anastahili pongezi kwa kuonyesha dira ya taifa.
Si siri. Hivi karibuni viinchi tena visivyojaa kwenye kiganja vimejaribu kuigeuza Tanzania ‘punching bag’ ya kubarehe kwake.  Viichi hivi vyenye matatizo kila aina vilifikia mahali hata kutishia kuwa ipo siku vitatushughulikia kana kwamba hili linawezekana.
Nani mara hii kasahau maneno ya kejeli toka nchi jirani ya Malawi ikidai eti Ziwa Nyasa ni mali yake pekee? Bahati nzuri Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, hakumng’unya maneno pale aliposema kuwa Tanzania haitaruhusu mtu kuichezea.
Hiyo ya Malawi tisa. Kumi ilikuwa ni pale nchi jirani ya Rwanda ilipoamua kutumia vyombo vyake vya habari na rais wake kututunishia misuli sababu ya kuwapa ushauri nasaha wa bure kuwa wazungumze na waasi wao ili eneo la Maziwa Makubwa liwe na amani.
Ushauri huu wenye kila ukweli na uhalisia ulitolewa na Rais Kikwete kule Addis Ababa kwenye kikao cha wakuu wa umoja huo mwishoni mwa mwezi Mei.
Ni bahati mbaya kuwa ushauri mulua wa rais Kikwete ulipokelewa vibaya kiasi cha rais wa Rwanda kumueleza kama mtu asiyejua anachosema ukiachia mbali kuwa mzembe wa kufikiri.
Haya si maneno ya kumtamkia mkuu wa nchi nyingine. Huu ni ukame kidiplomasia na kimkakati.
Baada ya Kagame kujigamba kuwa angemshughulikia Rais Kikwete siku ikiwadia alipohudhuria maafali ya Chuo cha kijeshi huko Kinama nchini Rwanda, Tanzania ilikaa kimya.
Baada ya hapo magazeti ya Rwanda yakiongozwa na lile la serikali la New Times yalishikilia bango na kuandika matusi na kejeli kila aina.
Gazeti hili liliamua kwa makusudi kupindisha ukweli pale lilipodai kuwa rais Kikwete alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje mwaka 1994 wakati yalipofanyika mauaji ya kimbari nchini humo yaliyosababishwa na kutunguliwa kwa ndege ya rais wa zamani wa Rwanda, Juvenal Habyarimana iliyodunguliwa ikitokea Arusha kwenye mkutAno wa kujadili amani ya Rwanda.
Licha ya kumuita Kikwete muuaji wa kimbari ‘genocider’, lilimuita mtetezi wa wauaji wa kimbari! This is more than too much. Halivumiliki. Rwanda ishukuru upole na huruma za Kikwete.
Haya yangelisemwa juu ya Nyerere historia ingeishaandika vinginevyo.
Wengi wanashangaa na kuhuzunishwa na upogo na upofu wa Rwanda. Swali kubwa linaloulizwa na wachambuzi wengi ni kwamba kama Rwanda ya kabla ya Kagame isingezingatia ushauri wa kuongea na waasi wa Rwanda Patriotic Front (RPF) wakiongozwa na Kagame mwenyewe wakati ule, Kagame angekuwa hapo alipo?
Je, kosa la Tanzania ni nini? Ni ile hali ya kutaka amani katika eneo zima au kufumbia macho kupotoshwa kwa itifaki kulikoshuhudiwa kwa kuruhusu rais wa zamani wa Rwanda kupanda ndege moja na wakuu wote wa serikali jambo ambalo ni kinyume?
Je, kosa la Tanzania ni kumtengeneza Yoweri Museveni, Rais wa Uganda aliyemtengeneza Kagame? Je, Rwanda inao ubavu wa kujipima na Tanzania?
Jibu la swali la mwisho lilitolewa hivi karibuni huko Kaboya, Kagera wakati rais Kikwete akihutubia wananchi kwenye kumbukumbu ya mashujaa.
Rais Kikwete alikaririwa akisema tena bila kumung’unya akisema, “Laleni usingizi salama. Msisikilize maneno ya mitaani, kwa sababu jeshi letu liko imara kabisa kulinda nchi yetu na mipaka yake.
Yeyote atakayejaribu kuivamia ama kuichokoza nchi yetu atakiona cha mtema kuni. Nchi iko salama na jeshi liko imara kulinda nchi yetu.
Kikwete alikwenda mbali na kusema kuwa wale wanaoota mchana basi wajirejeshe kwenye yaliyomkuta imla wa zamani wa Uganda, Idd Amin ambaye hakuchakazwa tu bali kuondolewa madarakani.
Kwa wenye akili huu ni ujumbe mzito wenye kuonyesha msimamo na dira ya taifa. Ni kweli. Tanzania si taifa lelemama la kuweza kuchezewa hata na vipande vya nchi vyenye matatizo lukuki.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 7 , 2013. 

Viewing all articles
Browse latest Browse all 3173