Quantcast
Channel: Free Thinking
Viewing all articles
Browse latest Browse all 3173

BASATA na Polisi acheni kujikomba

$
0
0
            Baada ya rais John Pombe Magufuli kutengua marufuku ya wimbo wa Wapo waEmanuel Elibariki aka Ney wa Mitego na kukamatwa kwake, tokana na katazo la Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na kukamatwa na jeshi la Polisi, tunaweza kusema kuwa sasa wanaojikomba na kujifanya wanajua hisia za rais wamekwama. Yaani mnakamata mtu bila kumpa onyo au haki ya kujitetea bado mnaona mnatenda haki kweli?
             Kwanza, ni aibu kwa taasisi zinazoendeshwa kwa fedha za umma kama Basata na Polisi kujikomba. Huu ni ushahidi kuwa taasisi hizi ima hazijui kazi zake zaidi ya kujigeuza vikaragosi vya kueneza woga na ujinga nchini au zinafanya kazi kwa woga usio na msingi ukiachia mbali kutaka kuwafurahisha wakubwa hata kama ni kwa kuwaumiza watu wasio na hatia.
            Pili, wapo waliopongeza hatua ya rais na kulaani hatua za Basata na Polisi. Kimsingi, hapa hakuna cha kupongeza hasa ikizingatiwa kuwa rais ndiye aliyeachia mambo haya kiasi cha kuyajengea mazingira hadi kujenga dhana nyingine kuwa nchi yetu inaendeshwa kwa woga na kupinda sheria hasa wanapoguswa wasiopaswa kuguswa au watu walio karibu na rais au hata kumgusa rais mwenyewe tokana  na mambo wanayotenda dhahiri.
            Tatu, sioni sababu ya kumpongeza rais kwa alichofanya hasa ikizingatiwa kuwa amejitahidi kukwepa aibu kwake na serikali yake ukiachia mbali kushtakiwa. Kama atajifunza tokana na kadhia hii litakuwa jambo la maana kwake na kwa taifa kwa ujumla. Haipendezi rais kuwa anaingilia kila jambo.  Kwanini rais hakuwaamuru Basata na jeshi la polisi au waziri anayehusika kutenguamarufuku ya wimbo wa Mitego na kushikiliwa kwake kinyume cha sheria? Sitaki rais wetu ageuzwe rahisi na wale wanasukumwa na woga na kujikomba kiasi cha kushindwa kusimamia sheria na haki. Nadhani baada ya rais kutengua uwaziri wa Nape Nnauye baada ya kuunda tume ya kuchunguza kashfa ya kuvamiwa kwa vituo vya Clouds, wanywanywa na woga walidhani hii ndiyo sera yake, kulindana, kutishana na kuumizana bila sababu.
            Nne, hata hivyo rais alitumia busura kuepuka serikali yake kuadhiriwa mahakamani. Hivyo, basi tokana na alichofanya rais,  Mitego ashitaki serikali kutaka afidiwe kwa mateso na athari alizozipata yeye binafsi na kazi yake ili liwe somo kwa wote wanaotumia madaraka vibaya kwa sababu za kulindana na masuala binafsi.
            Baada ya kusema haya, acha nimshauri rais Magufuli kuwa na subira linapotokea jambo japo si yote yanayotaka subira. Mfano, anapogundua kuna madudu yanayosababisha hasara kwa taifa, lazima achukue hatua za tahadhali mapema. Inapokuja kwenye masuala kama ukosoaji, rais anapaswa kuacha vyombo husika vitimize wajibu wake au kuingilia kwa kuwatumia wasaidizi wake badala ya kujiingiza kwenye mambo yasiyo ya hadhi yake kama kwenye kadhia hii ya Mitego ambaye bila shaka sasa anachekelea kuwa rais amemsaidia kuwa maarufu na kuonekana shujaa bila ulazima kama rais angekuwa anaacha walio chini yake waache kufanya kazi na maamuzi kwa woga.
            Sita, tunashauri wakuu wa vyombo husika waliotoa amri hizi za kijinga watajwe hadharani na kuwajibishwa mara moja ili liwe somo kwa wengine wenye kuendeshwa na woga na kujikomba kufanya maamuzi yao.
            Saba, kwa kuamuru wimbo wa Mitego uendelee kuchezwa, ni dalili kuwa sasa rais anaanza kuona madhara ya Bashite kwa utawala wake. Haiwezekani mtu mmoja tena asiyependa kujitetea wala kutoa ufafanuzi kuhusiana na tuhuma dhidi yake aliweke taifa rehani. Bashite ni nani katika Tanzania? Kwanini watendaji wetu wanakuwa wepesi kuwaadhibu watu wema wakati wakiwakingia kifua waovu? Hili halikubaliki tanzania. Kama ambavyo rais amekuwa akionya watanzania kuepuka kujenga mazingira yanayovunja amani nchini kwa kutolea mfano wa kilichotokea Rwanda mwaka 1994, vivyo hivyo, naye aepuke kupalilia hayo mazingira kwa kuwatendea watanzania kibaguzi na kiupendeleo kama ilivyo kwenye sakati la Bashite.
            Nane, uzoefu unaonyesha kuwa rais Magufuli hana mtu wa kudumu. Rejea alivyombadilisha Katibu Mkuu kiongozi, Ombeni Sefue hata baada ya kuwa amemhakikishia kuendelea kuchapa kazi lakini akamuondoa. Hata Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam ambaye yuko katikati ya kadhia hii anapaswa kuchukua tahadhali kuwa hakuna aliyeshindana na umma akaushinda. Angekuwa mkomavu kisiasa, angeachia ngazi kwa hiari yake ili lau umma umsamehe kama kweli alighushi hivyo vyeti na kuvamia Clouds.
            Tumalizie kwa kuwapongeza wote waliosimama kidete na kulaani ujinga uliokuwa umetendeka ambao ulionyesha wazi kuminywa kwa haki za kikatiba za watanzania za kutoa mawazo bila pingamizi wala kutishwa ilmradi wasivunje sheria. Hongera Ney wa Mitego kwa kutengua kitendawili cha Bashite ambacho kilianza kuwa donda ndugu na jipu kubwa tu lenye kumngoja rais alitumbue mara moja. Turudie, tanzania ni zaidi ya rais, Bashite na yeyote yule anayedhani ana haki ya kuwa juu ya wengine. Ni nchi ya kidemokrasia inayopaswa kuongozwa na sheria, kanuni na katiba chini ya matakwa na shuruti zote za utawala bora na wa sheria.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 3173