Quantcast
Channel: Free Thinking
Viewing all articles
Browse latest Browse all 3176

Tanzania aihitaji kuombewa bali kuambiwa

$
0
0
         Ninapoandika kuna kundi la matapeli wa majoho wanaoandaa tamasha eti la kuombea taifa! Hivi Tanzania inahitaji kuombewa au kuambiwa ukweli mchungu hasa kupambana na vikwazo vinavyoifanya iwe shamba la bibi na ombaomba duniani? Kwanini kuomba badala ya kuyakabili matatizo ya kweli yaani ujinga, umaskini, rushwa, ufisadi, usanii, ukondoo, ukijiko, ukuku na adha nyingine?
            Ni matapeli wengapi wamejificha kwenye uganganjaa kama kutenda miujiza wanaowaibia watanzania maskini na wajinga mchana hadi kugeuka matajiri wa kuktupwa kwa muda mfupi? Si tunawaona kila siku wakijipachika vyeo kuanzia uchungaji, uaskofu hadi udaktari? Nani aliwawekea mikono zaidi ya utapeli na njaa zao?
            Juzi wamejitokeza wengine eti wanabariki mafuta huku wakijifanya kumpenda rais John Pombe Magufuli ambaye huweka picha yake mbele kwa kisingizio cha kumuombea. Japo kuomba siyo jambo baya, kwani lazima mtangaze na kuitisha makongamano kama siyo kutaka kujiweka karibu na rais?  Kama tutaendekeza kuomba, kazi tutafanya lini? Hivi hawa wanaojifanya kuipenda Tanzania kiasi cha kuandaa matamasha na makongamano ya kuiombea, hawawezi kufanya maombi yao majumbani au makanisani mwao bila kutangaza kama siyo kutafuta kuwa karibu na rais?
            Sikumbiki Yesu kuandaa mkesha wa kuombea chochote zaidi ya kufanya kila alichoweza bila kutafuta sifa tena akiwaambiwa walionufaika na huduma yake wasimwambie mtu. Yesu hakutaka sifa wala makuu. Ndiyo maana hakuwa tajiri wala hakuwa na vyeo vya kujipachika na vya kughushi kama vile daktari zaidi ya kuitwa Mwalimu na wanafunzi wake.
            Kama tutakuwa wakweli kwa nafsi zetu, kweli Tanzania inahitaji maombi kama majibu ya matatizo yake? Mbona hatusikii nchi jirani zikiwekeza katika kuomba. Tunapaswa kufanya mambo kisayansi na kwa kuangalia ukweli na uwezekano badala ya ndoto na visingizio kama maombi. Kwanza, maombi hayatuhakikishii majibu ya tatizo kwa muda tunaotaka. Pili, maombi si njia yenye kuaminika ya kupambana na matatizo. Na tatu, tunaweza kuomba lakini kufanyike baada ya kazi na si kwa matangazo na kutafuta sifa kirahisi kwa baadhi ya walioko nyuma ya mradi huu wa sala ambao kimsingi, hauna uhakika.  Kuomba hakuna haja ya kugeuka kazi ya kundi fulani au watu fulani au dini fulani.  Kwa watu wanaoipenda nchi yao, bila shaka watakuwa wakiiombea kila siku kwenye maombi na sala zao iwe ni misikitini, makanisani hata majumbani. Hivyo, hawa wanaokuja na gea ya kuliombea taifa, wanapaswa kujua kuwa walichelewa kujua wajibu wao kama watanzania. Leo tutaanza kuombea taifa. Kesho  tutasikia kuliimbia. Na kesho kutwa tutasikia kulitoa sadaka. Dawa ya matatizo ya taifa letu si maombi bali kuambiana ukweli kuwa kuna wenzetu hawafanyi kazi na wengine wanawaibia watanzania  kwa kushiriki vitendo viovu kama vile ufisadi, biashara haramu ya mihadarati, ubabaishaji, utapeli na maovu mengine mengi ambayo yametamalaki. Kama kuna kitu taifa letu linahitaji, nadhani si kuomba bali kuambiwa ukweli kuwa tusipolipenda na kuchapa kazi, hata tuombe uchi au bila kukoma tutazidi kuumia. Hivi wanaoajiri wageni kinyume cha sheria nao wanahitaji maombi? Mateja nayo yanahitaji maombi? Wauza unga wanahitaji maombi? Polisi na maafisa forodha wanaowezesha wauza unga kupitisha mizigo yao hatari nao wanahitaji maombi kweli? Wanaotumia madaraka vibaya na wababaishaji wa kisiasa nao kweli wanahitaji maombi? Wanaotumia vyeo kuwaumiza, kuwakomoa na kuwachafua wapinzani wao nao kweli wanahitaji maombi? Wanaotukana viongozi wetu kweli nao wanahitaji maombi? Wanaofuja fedha na mali ya umma kweli wanahitaji maombi au kuambiana kuwa tupambane nao kwa udi na uvumba?
            Kuna njia zinazoingia akilini za kushughulikia matatizo yetu kama watu na jamii. Kwa mfano, tunapopambana na ukame, dawa si kuomba mvua tu bali kubuni namna ya kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji. Tunaposhindwa kuelewana, njia si kuomba bali kutafuta namna ya kuelewana. Tunapokumbwa na umaskini dawa si kuombeana tena kuombewa na wale wanaotufanya maskini ima kwa kula bila kufanya kazi au kuwaibia maskini bali kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa. Kutofanya kazi lakini baadhi yetu wakatakea kuwa matajiri bila maelezo ni dalili za ufisadi ambao kimsingi, ndicho kikwazo kikubwa kwa taifa letu.
            Hakuna taifa lililopata maendeleo kwa njia ya kuomba iwe ni misaada au maombi zaidi ya uchapa kazi. Kwa vile sera ya rais Magufuli ni ‘Hapa Kazi Tu’ namshauri awaulize hawa wanaopoteza muda na fedha nyingi wakiandaa makongamano na matamasha ya kuombea taifa, wafanya kazi kwanza; maombi baadaye. Anachoweza kufanya rais kulisaidia taifa ni kuwachunguza wote waliojipachika vyeo vya kidini na vinginevyo wenye utajiri wa kutisha ili watumbuliwe.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 3176