Quantcast
Channel: Free Thinking
Viewing all articles
Browse latest Browse all 3173

Serikali izuie bendera madhabahuni na vyeo bandia

$
0
0
Image result for tanzanian flag
 
              Kwa walioangalia mahubiri ya Josephat Gwajima baada ya kuachiwa toka Central police station, watakubaliana nami kuwa ana bendera ya taifa na ya Israel kwenye jukwaa lake. Siku zote tunaonywa kuchanganya dini na siasa. Je huyu anayetumia bendera kwenye mambo ya kidini wakati hana stahiki ya kuwa na bendera anadhamiria nini? Je kama makanisa na misikiti yote watafanya hivyo, tofauti ya dini na siasa ambayo Tanzania imeitengeneza itakuwapo?
            Hata ukisikiliza mengi ya mahubiri ya Gwajima ni ya kisiasa. Cha mno anajaribu kujipigia debe ili kuwa karibu na rais John Pombe Magufuli ambaye hata hivyo anaonyesha msimamo wa kutotaka kuchezewa. Ni ajabu kuwa Gwajima amekuwa mwepesi wa kusahau kuwa ni jana tu alikuwa shirika la Edward Lowassa dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Sasa baada ya mtu wake kushindwa, Gwajima anajitahidi kwa kila hali kujifanya anampenda na kumuunga mkono Magufuli kwenye wakati wa kuvuna wakati alimpiga kiatu kwenye kulima (uchaguzi). Je Gwajima anadhani kuwa Magufuli naye ni msahaulifu au msanii kama yeye?
            Ukiangalia ujio wa Gwajima na wenzake kama yeye waliojivisha vyeo vikubwa vya kidini, unagundua mambo mengi mojawapo likiwa ni kutojiamini. Wakati umefika wa kuondokana na viongozi wa kidini wa kujipachia madaraka ili kuepusha watu wetu kuzidi kuibiwa na kutapeliwa tokana na ujinga na shida zao. Kimsingi, kinachoendelea nchini licha ya kuwa ushirikina, ni ufisadi wa kiroho ambao madhara yake ni makubwa sana. Mtu asiye na shahada hata ya kwanza anaamka na kujiita daktari na lecturer na mamlaka zinamvumilia. Hili haliwezekani. Serikali zilizopita tokana na kuongozwa na watu wasioelimika na kusoma vilivyo, ziliwavumilia wasanii hawa kiasi cha kutosha. Magufuli daktari wa falsafa anajua uchungu wa elimu. Hivyo, tunamshauri atumbue ufisadi huu. Kwanini kwa mtu kujiita mheshimiwa Mbunge lazima achaguliwe au ateuliwe lakini si kwa askofu na vyeo vingine vya kiroho? Tunajenga taifa la namna gani kwa kuruhusu udhalilishaji wa taaluma? Je hatutoi motisha kwa watu kudharau elimu na kutafuta vyeo na stahiki za kisomi hata kwa njia ya kughushi ambalo ni tatizo kitaifa linalowahusisha wanasiasa wengi; na sasa viongozi waroho wa kiroho wa kujipachika? Kwanini wanaojifanya madaktari wa kutibu watu wanakamatwa na kufunguliwa mashtaka wakati matapeli wanaojiita au kupeana udaktari uchwara wanaachiwa? Nadhani waziri wa Elimu anapaswa kuliangalia hili kwa makini hasa ikizingatiwa kuwa naye ni msomi wa kumenyekea na si wa kupewa.
            Japo ni kielelezo cha ujinga wa aina yake kwa mtu asiyesomea shahada yoyote kujipachika shahada husika, kwa wajinga na vihiyo hili si tatizo. Kuwasaidia ni kuhakikisha hakuna mtu anaruhusiwa kutumia cheo cha heshima wala kujipachika au kughushi. Kwanini wachungaji kama hawa wa kujipachika hawakuwapo wakati wa utawala wa Mwl Julius Nyerere? Jibu ni rahisi kuwa Nyerere hakuruhusu ujinga na ufisadi kama huu wakati wake kwa vile alikuwa ameelimika na kusoma vya kutosha.
            Tukirejea kwenye suala la kutundika bendera, bendera ina stahiki na namna za matumizi yake. Wapo maafisa wa serikali walioruhusiwa kutumia bendera ya taifa kama alama kuu ya utaifa wetu. Sasa hawa wachunaji wamepewa na nani mamlaka na kwa sheria gani kutumia bendera yetu kwenye shughuli zinazotia kila aina ya shaka ukiachia mbali kuwa si wote wanaoamini kwenye maigizo yao? Kuna taasisi zinazoruhusiwa kupeperusha bendera ya taifa kama vile ofisi za serikali, taasisi za umma kama vile shule na nyinginezo lakini si makanisa wala misikiti; kwa vile taifa letu halina dini japo linaundwa na watu wenye dini tofauti na kinzani. Hatuwezi kuruhusu wafanya biashara ziwe za bidhaa au kiroho watumie bendera yetu. Kufanya hivyo, licha ya kuidhalilisha ni kubariki biashara hizo hata kama nyingine ni haramu. Siku hizi dini umegeuka uchochoro wa kila tapeli kupatia mkate wake. Tutaishi kwa mahubiri kweli? Nashauri serikali itenge mahubiri kuwa ni jumapili na ijumaa. Zaidi ya hapo wahusika lazima walazimishwe kufanya kazi nyigine. Wale waliojipachika wasimamishwe haraka ili kuepuka utapeli huu kuendelea kuumiza watu wetu wengi wajinga na washirikina. Ni ajabu katika karne ya 21 bado kuna watu wanaaminishwa kuwa kuna anayeweza kutenda miujiza wakati miujiza yenyewe ni kuwaibia na kuwageuza majuha wa kawaida tu kama si mabuzi ya kuchunwa. Huwa nasema kila mara kuwa Yesu licha ya kuwa maskini, alisema tajiri hawezi kuuona ufalme wa mbinguni. Rejea kisa cha Zakayo. Ajabu ya maajabu leo wachunaji wengi ndiyo wakwasi wa kutupa. Je wataweza kuwatumikia mabwana wawili yaani mali na Mungu kweli wakati Yesu wanayejidai kumhubiri alishaweka mambo sawa? Je nani anamdanganya nani hapa?
            Tumalizie kwa kuishauri serikali imalize kadhia hii ambayo wachunaji wengi wameitumia kujipatia utajiri wa haraka ama kwa kufaidi misamaha ya kodi au kuwaibia watanzania wajinga na maskini wenye matatizo wasiojiamini. Hali imekuwa mbaya hadi matapeli wanaosifika toka kwenye mataifa kama Nigeria wamejipenyeza kwenye nchi yetu chini ya kivuli cha kuhubiri. Enough is enough.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili kesho.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 3173