Hivi karibuni, baada ya kubainika kuwa watanzania wanaochukua uraia wa kigeni hupotgeza haki muhimu ya kumilki ardhi, kumekuwapo mjadala kwenye mitandao ya kijamii. Tokana na unyeti wa suala zima, napenda kutoa maangalizo yafuatayo kama mwana diaspora:
Kwanza, nilishangaa kuona kuwa bado tunaendelea kuwa na mawazo ya kijima ya wakati wa vita baridi ambapo nchi za magharibi na mashariki zilitutengeneza kuwa kama maroboti yenye kushikiana na kuchukiana bila hata kujua ni kwanini. Zama zile tuliogopa na kukata uraia pacha kwa hofu ya kuweza kuingiza wapelelezi na mawakala wa maadui zetu kutuchunguza na kuhatarisha usalama wetu. Je kwa sasa tunahofia nini zaidi ya kutumia mabaki ya ukoloni (colonial carryovers)? Ajabu, wakati sisi tunabaniana uraia pacha, wale waliotutawala na kutujengea shaka na uadui wanaruhusu! Ukiachia hili, sisi tuna nini cha kuhofia wakati ni nchi tegemezi zilizoharibiwa kiasi cha wananchi wake kuzikimbia kutafuta riziki kwingine?
Pili, inapaswa kufahamika kuwa wakati sisi tukisuasua na kubaniana uraia pacha, nchi tajiri hazizuii wageni waliochukua uraia wao kubaki na uraia wao wa kuzaliwa. Kama ni kuogopa kuhujumiwa basi hizi ndizo zingeogopa hili kwani zina mali na fedha nyingi za kupoteza. Nchi nyingi za kiafrika zinategemea fedha inayotumwa na wana diaspora. Kwa mfano gazeti la Mail and Guardian (2 Juni, 2015) linaripoti kuwa nchi za Eritrea zinategemea pesa toka kwa diaspora kwa kiasi cha 38%, Cape Verde, 34%, Liberia , 26%, na Burundi 23% ikilinganishwa na pato la taifa. Hii si pesa kidogo na rahisi kwa nchi kuipata. Japo sina takwimu za Tanzania inaingiza kiasi gani, kutokana na uzoefu binafsi, najua inaingiza fedha zinazoweza kuelezwa kuwa zinakwenda kwa watu binafsi. Huu ni ushahidi kuwa wana diaspora wana mchango mkubwa kwa nchi zao jambo ambalo linapaswa kuwa kama njia mbili yaani nipe nikupe (twoway traffic).
Tatu, kuonyesha kuwa bado tunaendelea na mawazo ya kijima, kuna taarifa nyingi toka Tanzania ambapo wageni wanaopewa uraia wa Tanzania huwa hawabanwi kama watanzania wanaochukua uraia wa kigeni. Wengi wa wageni hawa hubaki na uraia wao kiasi cha kutumia status hii kuifilisi na kuiibia Tanzania wakati ikuzuia wazawa wake kuwa na uraia pacha. Mifano ya wahalifu walioibia Tanzania mabilioni ya fedha kama vile Chavda Group ambaye mwaka 1993 aliyetumia mashamba ya mkonge kukopa fedha na kuyatelekeza na Saileth Vithlania wa kashfa ya rada inaweza kukueleza hali ikoje ukiachia mwingine wa hivi karibuni Hermant Patel aliyejitwalia ardhi ya Tanzania ipatayo hekari 35,000 na kwenda ulaya kwenye mabenki kuiweka kwenye poni. Je tunamkomoa nani; na ili iweje au ni kwa vile matapeli na wahalifu wa kimataifa wanashirikiana na maafisa wa juu wa serikali kama ilivyokuwa kwenye kesi mbili hapo juu?
Nne, sheria ya ardhi ni kimeo. Inawazuia watanzania waliochukua uraia nje kumilki ardhi wakati ikishindwa kuwadhibiti waliochukua uraia wa Tanzania kuutumia kuiibia kama tulivyoonyesha hapo juu. Je mhusika akiwa na makaburi ya wazazi wake nayo serikali itayachukua? Je kwa zuio hili, ni busara kwa diaspora wenye uraia wa kigeni kuwekeza Tanzania wakati hawakubaliki? Mbona nchi nyingine za kiafrika kama Rwanda zimeruhusu uraia pacha? Nadhani Tanzania bado tuna mawazo ya kizamani ya enzi za vita baridi.
Nini kifanyike?
Kwanza, kushawishi serikali ya Tanzania kuruhusu uraia pacha au kuzi-lobby nchi zilizoendelea zilizotoa uraia kwa watanzania kuhakikisha watu wao wanapodhulumiwa ardhi nazo zisitishe misaada na ushirikiano hata ikiwezekana kuingilia kati.
Pili, kuna haja ya kujiuliza: Kwanini watanzania wanachukua uraia wan je? Wanafanya hivyo ili wapate fursa ambazo hazipo nyumbani. Serikali ambayo inapaswa kulaumiwa kwa kushindwa kuweka mazingira mazuri kwa watanzania kupata fursa kama hizi haipaswi kupewa mamlaka ya kuamua nani awe na uraia pacha au la. Kwani, kimsingi, serikali ndiyo chanzo cha haya yote. Watu wanataka elimu bora, maisha safi, kuaminika wanapotaka kusafiri nje na mengine mengi tu. Wekeni mazingira bora kwanza ndiyo mkataze watu kuwa na uraia pacha. Mbona nchi tajiri zenye kila huduma bora zinawaruhusu watu wenu kuchukua uraia wao, kufaidi huduma zao na hata kutuma fedha huko wanakonyimwa uraia pacha?
Tatu, kwa mjibu wa mtandao wa dualcitizenshipmalawi.blogspot.ca nchi zipatazo 23 za kiafrika zinaruhusu uraia pacha. Hivyo, Tanzania inapaswa kujifunza toka kwa nchi kama hizo tena jirani kama vile Kenya na Rwanda zinazoruhusu uraia pacha na namna zinavyofaidika nao ikilinganishwa na kuupiga marufuku. Bila kubadilika, Tanzania itajikuta inaruhusu raia wa nchi jirani ambao watatumia fursa ya kujipatia ardhi Tanzania na kubaki na uraia wao huku watanzania wa kuzaliwa wakinyimwa ardhi. Rejea kilichotokea baada ya RPF kuchukua madaraka nchini Rwanda, wanyarwamnda wengi waliokuwa wamepewa uraia wa Tanzania waliutelekeza na kurejea kwao bila kizuizi cha kuhitaji kuomba upya kama ilivyo kwa Tanzania ambayo ilikula hasara kwa kuwasomesha na kuwatunza tangu wengine wazaliwe hadi walipoondoka.
Nne, Tanzania iache kupoteza muda kuwazuia wananchi wake wa kuzaliwa uraia wa pacha wakati ukiugawa kama njugu kwa matapeli wa kimataifa wanaoutumia kuhijumu tofauti na wana dispora wanainufaisha kwa kutuma fedha kwa watu wake. Pia ifahamu kuwa Afrika kwa mtu yeyote mweusi ni mama ambayo hakuna namna yoyote ya kuitenganisha na watoto wake kwa sababu za kijima na wakati mwingine hata ujinga na roho mbaya. Kwanini wakenya na wanyarwanda, kama si roho ya korosho waweze Tanzania ishindwe? Nadhani uraia pacha ni haki na si suala la nani watake au kutoa kama ofa. Wote tunahitajiana. Rekebisheni kinachowasukuma watu wenu kukimbilia nje uone kama kuna atakayelalamika.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.