MAKALA ya mwandishi George Maziku yenye kichwa cha habari “Wanaopinga Tanganyika walaaniwe’ iliyochapishwa katika gazeti hili toleo lililopita, haiwezi kupita bila kuweka mambo sawa. Kwanza, hakuna haja ya kulaaniana, kuchukiana wala kudharauliana bali kujadiliana kwa hoja zenye mashiko na ushawishi. Pia hakuna wanaopinga kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika bali umuhimu na gharama zake. Nadhani mleta hoja ameshindwa kubaini ukweli uliojificha kwenye gharama. Maziku anaweza kuwa na hoja ila lugha na namna alivyoileta imepoteza hoja. Pili, ni vizuri kufahamu kuwa kila Mtanzania ana haki kidemokrasia kutoa mawazo yake hata kama hatuyapendi. Tatu, tukubaliane kuwa kuendeleza u-mimi wa kila upande na serikali yake ni upogo na unafiki unaofanya tuungane shingo upande. Kama tunalenga kuleta maendeleo kwa watu wetu, basi tunapaswa kuepuka gharama zisizo za lazima kama kuwa na serikali tatu. Nne, tuzisikilize na kuzijadili hoja za wasiopenda kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika. Nadhani ni hoja yenye mashiko kupendekeza kuwa tuunganishe nchi iwe moja badala ya kuwa na utitiri wa serikali ambao utambebesha mzigo mlipa kodi maskini wa taifa hili. Ingawa mashabiki wa Tanganyika wanashindwa kuelewa kuwa wanachohitaji Watanzania si wingi wa serikali bali maisha bora, tusiwakatie tamaa. Tuwaelimishe. Naamini kuna siku wataelimika na kuelewa kilichoko nyuma ya ujio wa Serikali ya Tanganyika. Tano, tutatoa sababu za kwanini Serikali ya Tanganyika si ‘big deal’ na hakuna mwenye kujua mahitaji ya Watanzania ambaye anaweza kuiunga mkono. Sita, serikali tatu itaongeza gharama za kiundeshaji kiasi cha kuwakamua na kuwafanya Watanganyika wawe maskini zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa ndio watakaokamuliwa pesa ya kuiendesha. Saba, kama ambavyo imekuwa Serikali ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar ambayo tangu kuungana imeendeshwa kwa pesa ya Watanganyika kutokana na ukweli kuwa Zanzibar haina vyanzo vya mapato ya kutosha kujiendesha kwa kiwango cha sasa. Nane, ujio wa Serikali ya Tanganyika utaua Tanzania. Hii ni kutokana na ukweli kuwa sasa tutakuwa na Wazanzibari ambao hawajawahi kukubali kuwa ni Watanzania na Watanganyika. Je, hapa Watanzania watakuwa wapi kama siyo kubakia kwenye makabrasha na vitabu vya historia? Tisa, kuanzisha Serikali ya Tanganyika ni kwenda kinyume na dhana na dhamira nzima ya Muungano ambao ulilenga kuwa na serikali mbili kuelekea moja, na si tatu kama watu wengi wasiopoteza muda kuisoma historia wanavyodhani. Kumi, kutaanza kuwepo utoroshaji wa mali za Tanganyika kuelekea upande mwingine chini ya dhana ya urais na utaifa mpya. Nadhani wanaopendelea serikali tatu wanasahau kuwa tukishakuwa Watanganyika na Wazanzibari kikatiba, watu wa upande wa pili wataanza kufanya mambo kama ambavyo majirani zetu wangetaka kufanya kwenye muungano wa Afrika Mashariki - kila mtu kuchuma na kupeleka kwao. Kumi na moja, licha ya kumfanya Mtanganyika kuwa punda kihongwe mwenye kubeba zigo la serikali utitiri na maskini, serikali tatu zitadhoofisha uchumi wetu na kuongeza kiwango chetu cha utegemezi kwa wafadhili. Tujuavyo, watawala wetu wa sasa hawana mpango wowote wa kuwa na serikali inayojiendesha yenyewe bila kutegemea kuombaomba na kukopakopa. Hebu tujiulize. Kama deni letu linaumuka kwa kiwango cha kutisha kwa sasa chini ya serikali kubwa mbili tulizonazo, hali itakuwaje baada ya kuwa na serikali tatu? Nani anapenda kuendelea kuwa tegemezi jambo ambalo ni hatari kwa heshima, mustakabali na uhuru wetu? Kumi na mbili, turejee kwenye makala ya Maziku. Anasema; “Ni jambo la kushukuru Mungu kwamba Tume ya Warioba imeheshimu maoni ya Watanzania walio wengi, waliotaka mfumo mpya wa Muungano wa serikali tatu kwa kuirejesha Serikali ya Tanganyika.” Si kweli kuwa wanaotaka serikali tatu ni Watanzania walio wengi. Kama wapo wengi basi watakuwa Wazanzibari au ni wa kubuni. Sijui Maziku anaweza kutwambia ni asilimia ngapi ya Watanzania wanaopenda kuwapo kwa serikali tatu na wasiopenda. Hili ni hitimisho la haraka na jumla linalokosa umakini na uchunguzi wa kina. Pia ifahamike kuwa wingi wa wanaounga au kupinga ujio wa Tanganyika si hoja. Hatuwezi kutumia falsafa ya ‘vox populi vox dei’, yaani wengi wape hata kama wamekosea. Mbona mwaka 1992 Watanzania wengi walipendelea kuendelea kuwapo mfumo wa chama kimoja kwa kukosa kusoma alama za nyakati, lakini busara za Mwalimu Julius Nyerere kujua kuanguka kwa ukuta wa Berlin zikatumika kuwasikiliza wachache? Tungekuwa kila siku tunasikiliza wengi hata kama hakuna ushahidi, basi kuna mambo mengi ya kijinga yangepitishwa kama ilivyo kwa sasa bungeni ambako wabunge wengi ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hupitisha vitu vya hovyo kwa wingi wao. Hivyo, tungeshauri tujenge hoja na kujadili hatima ya taifa letu kwa kuangalia mahitaji ya wakati badala ya zana chovu na za kizamani kama wengi wape. Japo Maziku ameongelea mengi kama ukubwa wa serikali, kwa nukta hizi kumi na mbili tuhitimishe mjadala kuwa hakuna haja ya kulaani wanaopinga uwepo wa serikali tatu. Tuwasikilize, tujibu hoja zao kwa hoja zenye mashiko tukizingatia uwezo wetu wa kiuchumi na utashi na ‘spirit’ ya kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar. Tunashauri akina Maziku wajitenge na hukumu za jazba na jumla. Mara nyingi huua hoja tena zinaweza kuwa za msingi. ChanzoL Tanzania Daima Julai 3,2013. |