Na Ansbert Ngurumo
RAIS Barack Obama, anaingia nchini Tanzania kesho mchana. Sihitaji kueleza nini kinaendelea hapa nchini kuhusu maandalizi ya mapokezi ya kiongozi huyo.
Yamesemwa mengi na kuandikwa mengi. Haya yanayoendelea mbele ya macho yetu na watawala wetu yanatosha kuitwa matusi dhidi ya utu wetu.
Iwe tulimwalika au alipanga mwenyewe kuja, kinachoendelea ni matusi zaidi ya yale yanayowahangaisha polisi wetu na kuwafanya wawakamate wanasiasa wa upinzani kuwa wanawatusi watawala.
Ndugu yangu mmoja ameniambia kuwa alipokuwa kijana wa shule moja ya sekondari mkoani Tabora, alipata fursa ya kuwa miongoni mwa vijana wachache waliochaguliwa kumpokea Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipotembelea Mkoa wa Tabora.
“Kama ilivyo kawaida, kulikuwa na maandalizi ya mapokezi ya Baba wa Taifa, wakati huo akiwa katika mwaka wake wa mwisho wa kuongoza taifa letu kama rais.
“Alifika eneo la mapokezi akitokea uwanja wa ndege, na burudani kadhaa zilifanyika; kisha akapewa nafasi kusalimu wananchi kabla ya kuingia ndani kwa ajili ya vikao vya ndani. Kama kawaida hakuchelewa kupiga vijembe palepale.
“Akawashukuru wananchi kwa kufika kumpokea. Kisha akasema; ‘Kwa niaba ya miti hii na mawe haya yaliyopigwa rangi, napenda kuwashukuru viongozi wa mji wa Tabora.’
“Akasema mawe yale na miti ile haijafanyiwa usafi muda mrefu lakini sasa kwa ujio wake vimepata fursa ya kupigwa rangi na kumwagiwa maji. Wananchi waliangua kicheko kikubwa.
“Kisha akarusha kijembe kingine kilichowauma viongozi wa mkoa. Akasema yeye hapendi harufu ya rangi inayopakwa kwenye kuta na mawe kama njia ya kupamba na kufanya usafi.
“Akasema anasikitika kuona viongozi wanang’ang’ania kupiga rangi kila mahali anapokwenda wakidhani wanamfurahisha, wakati kimsingi wanamkera sana. Hakuna aliyepiga makofi.”
Hadi hapa nani zaidi kati ya Obama na Nyerere? Wamarekani wameamua kututusi nasi tumekubali. Wamejenga hoja kuwa hapa si salama, kwa hiyo inabidi wao wenyewe wachukue jukumu la kumlinda rais wao na kutufukuza sote mjini.
Wao wamegeuka wenyeji, sisi tumegeuzwa wageni, tena wageni hatari kwa sababu wote kwa pamoja bila kujali nafasi zetu tunazotambiana nazo, tunaonekana ni magaidi mbele ya Wamarekani na rais wao.
Lakini ukweli usemwe, hivi wapi ni salama kati ya New York na Dar es Salaam? Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini aliwahi kuwatibua Wamarekani katika mdahalo mmoja uliohusu usalama.
Aliwaambia Wamarekani kuwa alikuwa anajisikia salama akiwa Soweto kuliko akiwa New York. Alipoulizwa sababu alisema watu wengi wa Marekani wanatembea na silaha mifukoni mwao, kwa hiyo kuna silaha nyingi mitaani, kwenye treni, mabasi na hata kanisani.
Akasisitiza kuwa idadi ya silaha nyingi zilizo mitaani hata kama zina leseni, kwake ni tishio la usalama.
Rais Obama, iwe amekaribishwa kwetu au amejileta mwenyewe, wengi tulidhani ni mgeni wa kuishia sebuleni. Kinachoendelea sasa ni kama anatulazimisha tumkaribishe chumba cha kulala. Kwa ujio wake hakuna siri ya taifa itakayobaki bila kuwekwa wazi mbele yake.
Tumesikia waheshimiwa wetu waliozoea kupigiwa mizinga 21 na kutandaziwa zulia jekundu. Lakini safari hii ni makachero wa Obama watakaoamua nani aingie kumpa shikamoo Obama Kada na Mbunge wa CCM, Kapteni John Komba, aliwahi kuimba wimbo uitwao: ‘MGENI’. Katika wimbo huo anaeleza mgeni alivyoingia chumbani na kumwaga upupu. Matokeo ya upupu huo, baba na mama wanajikuna.
Obama anataka kuingia chumba cha kulala ili afanye nini huko? Mbona rais wa China amemtangulia? Mwanamwali wetu atakuwa salama kweli? Simaanishi Salma, namaanisha mwanamwali wetu wa taifa, yaani gesi, dhahabu, pembe za ndovu na tanzanite.
Kwa nini hataki kusubiri tumletee sokoni au angalau sebuleni? Anaingia chumbani kutafuta nini? na ‘kitanda’ hicho kitalaliwa wangapi?
Waafrika tunaruhusu mme mmoja, wake wengi; lakini si mke mmoja waume wengi! Hii mila yetu hivi sasa inapigwa vita lakini inavumilika.
Hii ya mwanamwali wetu wa taifa kugombaniwa na wanaume wengi itatuletea upupu, kwa sababu waume wengine wanaoingia huko ‘hata kupima hawajapima!’
Tena kwa Obama ni hatari zaidi kuingia chumba cha kulala, kwa sababu tumemsikia huko Senegal akipigia chapuo ushoga.
Asivyo na dogo, na kwa jeuri hii ya Wamarekani, Rais Obama anaweza kurudia kauli hiyo hapa Dar es Salaam, tena akasindikizwa na vicheko na tabasamu za watawala.
Kwa tabia yake hiyo ya kushabikia ushoga, kuna hatari akaingia chumbani na kumfukuza bibi harusi, ili abaki na baba yetu. Je, atakuwa salama?
Yawezekana lugha hii ya kishairi ikawauma baadhi ya wasomaji, hasa watawala na maswahiba wao. Lakini huu si utani.
Tumevuliwa nguo, tumedhalilishwa. Utu wetu umeondolewa kwa hiari ya watawala wetu. Kumbe haya ndiyo madhara ya kutembeza bakuli bila kikomo.
Tumekuwa tunashangilia kumwona rais wetu akishinda na kulala kwenye ndege, huku akidai anakwenda Ulaya, Asia na Marekani kuhemea.
Sasa ulaji umegeuka ‘uliwaji’. Kwa hakika tumeliwa na kugeuzwa kitoweo. Na sasa hawataki kulia kitoweo hiki sebuleni, bali chumba cha kulala. Tukubali kudhalilika kwa kiwango hicho? Na bado tunadai sisi ni raia wa nchi huru?
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili Juni 30, 2013