Quantcast
Channel: Free Thinking
Viewing all articles
Browse latest Browse all 3175

Tamaa, upofu, uroho na roho mbaya vitaliangamiza taifa

$
0
0
MATUKIO  ya kushambuliwa kwa mkutano wa CHADEMA kule Soweto Arusha na kupigwa na kuumizwa vibaya kwa wananchi wakiwamo viongozi wa chama hicho hayawezi kupita bila kulaaniwa kwa sauti kali. 
Tanzania ilisifika kuwa kisiwa cha amani. Kwa sasa bila shaka inaanza kusifika kama kisiwa cha vurugu, ubabaishaji, ufisadi, kujuana, kulindana, kukomoana  na hata kudhulumiana.  Hivi ni dhuluma kiasi gani kwa kikundi fulani chenye kuamini kuwa madaraka ni staili yake kuwaumiza na kuwahujumu wananchi wasio na hatia? 
Ni upuuzi na ukosefu wa akili kiasi gani kwa kikundi kidogo cha watu kujiona kama ndicho chenye kujua na kumiliki kila kitu hata ikiwamo akili?
 Je kwanini sisi kama taifa hatutaki kujifunza toka tawala ovu na zandiki zilizofanya haya lakini bado zikaangushwa kwa aibu na kejeli? Walikuwapo akina Muamar Gaddafi (Libya), Hosni Mubarak (Misri) na Saddam Hussein (Iraki). 
Waliogopewa sana na kuamini kuwa wao na waramba viatu wao waliumbika kuwatawala na kuwanyonya wengine wasijue arobaini yao ilikuwa imewadia. Kwanini hatupendi kusoma alama za nyakati kuwa wakati tulio nao si ule wa mwaka 47 ambapo kikundi kidogo cha watu kingeweza kuteka taifa na kulitenda litakavyo? Ni vizuri kutambua kuwa vijana wa sasa si wa kuburuzwa kutishwa wala kuchezewa mahepe.
Ni ajabu kuwa tumegeuka taifa la wakandamizaji na wababaishaji kirahisi hivi. Nani hajui kuwa kwa sasa tumo msambweni tukielekea kuzimu ambapo ulaji umechukua nafasi ya huduma? 
Leo tunaambiwa kwa mfano deni la taifa linazidi kuumka huku wahusika wakitumia kwa hisrafu na kuiba kama vile hakuna kesho. 
Nani hajui, kwa mfano, kuwa hoja ya  kurejesha fedha zilizofichwa Uswizi imeuawa kwa vile wahusika ni wakubwa au marafiki zao. 
Je ni kosa kuyashupalia haya? Je ni kosa kudai ukombozi? Je kupiga mabomu mikutano au kukata watu mapanga kwa vile wanapinga dhuluma ni jibu? 
Hata wenzetu wanaolia na kukumbuka maafa kama Rwanda walianzia huku. Hakika hawa walipaswa kuwa somo kwetu.
Inashangaza kuona kuwa Tanzania imegeuka nchi ya kulipuliwa na mabomu ya kigaidi na hakuna anayekamatwa kwa vile wahusika wana watetezi wao wenye mamlaka. Tunasema hivi si kwa chuki wala uchochezi bali kujibu kilio kilichotolewa na wahanga kule Arusha kuwa walimuona aliyerusha bomu na kutaka kumkamata lakini polisi wakamkingia kifua na kumtorosha. 
Je kama polisi na huyu gaidi lao si moja walimtorosha ili iweje kama siyo kuficha ushahidi? 
Laiti wangemtorosha kunusuru uhai wake ili ahojiwe na kuwataja wenzake ingeingia akilini. Ajabu badala ya kushughulikia kuwasaka waliolipua bomu, polisi inawashughulikia CHADEMA. 
Hali ni mbaya na yenye kutia kinyaa hadi kufikia baadhi ya walevi wa madaraka kusema eti waliolipua bomu ni CHADEMA ili kupata huruma ya wananchi. Hoja dhaifu  na ya aina yake kwa uhovyo. 
Yaani CHADEMA wawaue viongozi wao ili iweje na hiyo ‘huruma’ iwasaidieje kama siyo utaahira wa aina yake? Waingereza wana msemo : Go tell it to the birds. 
Tunadhani badala ya kuingiza siasa kwenye mambo nyeti na mazito kama mashambulizi haya ya kigaidi, serikali iwajibishwe kutuletea wale waliotenda uovu huu. Inashangaza kuona Watanzania wanageuka mateka kwenye nchi yao huku wakiuawa na kuteswa kutokana na kukataa kwako kulala kitanda kimoja na uovu. 
Wako wapi waliomteka na kumtesa Dk Steven Ulimboka na Absalom Kibanda? 
Wako wapi waliomuua Daud Mwangosi? Kwani hawajulikani?
 Je nani anahangaika kuwakamata iwapo walitumwa kutekeleza amri za wakubwa zao walioishiwa? 
Je hili ni jibu na hali itaendelea hivi hadi lini? 
Tumegeuka taifa la kulalamika lalamika. Ni jukumu la wananchi kujiletea ukombozi na kuhakikisha hatima zao zimo mikononi mwao. Tuwawajibishe watawala wetu waache kutuchezea.
Hakuna kitu kilitushangaza kama matamshi ya kizembe  kama yale yaliyotolewa na Waziri wa Nchi  Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) aliyekaririwa hivi karibuni akirusha lawama kwa wahanga akidai kuwa kumekuwapo na tabia ya wananchi kuchukia jeshi la polisi. Lukuvi anayetuhumiwa kughushi vyeti na sifa za kitaaluma ameonyesha ukweli kwa mada hii. 
Hivi Lukuvi hajui kuwa wananchi wanachukia jeshi la polisi kutokana na kushindwa kuwahudumia?
Ameshindwa kutambua kuwa wananchi wanaona kila uchao  mauaji na manyanyaso yanayotekelezwa na polisi huku wakilipwa kwa kodi za hao hao wanaowaua kama Swala mbugani? 
Imefikia mahali hata wanyama pori wana amani kuliko Watanzania. Je Lukuvi alitaka wananchi wawapende polisi kwa kuendelea kuwaua na kuwadhulumu? 
Je huku ni kufilisika kimawazo kiasi gani? Wengi walidhani kuwa wasemaji ambao ni makada wa chama tawala angalau wangekuwa wastaarabu wakatoa hata salamu za rambirambi badala ya kutonesha donda. 
Kwanini hawajifunzi toka nchi ambapo vyama tawala vilipigwa teke na kutokomea kwenye kaburi la sahau?
Tuhitimishe kwa kulaani kitendo cha wanasiasa uchwara kutetea ugaidi kwa vile unawanufaisha wao baada ya kuishiwa kisiasa. 
Hata hivyo wafahamu kuwa Watanzania si mataahira wala mawe yasiyobadilika. Kuna siku yaja watalia na kusaga meno. 
Kama taifa na jamii tusipoangalia tamaa, upofu, uroho na roho mbaya vitaliangamiza taifa. Tafakarini.
Chanzo Dira Juni27, 2013.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 3175