Baada ya kugundua na kushuhudia kuwa kuombea Kaya imekuwa fasheni ukiachia njia ya siri ya wahusika kujisogeza karibu na wenye ulaji na kuchangisha sadaka nyingi. Kwa mlevi huu ni mkenge ambao lisirikali na Kaya kwa ujumla vinapaswa kuuepuka kwa gharama zote. Mbali na kuwasogeza wahusika karibu na wenye ulaji, mkenge huu husaidia kuwafanya wahusika kupata umaarufu kwa mgongo wa wanasiasa maarufu kama rais. Utakuta wengi wakitafuta nafasi adimu ya kupiga picha na wazito wa serikali kama vile rais –ambaye hata hivyo, haonyeshi kushabikia ujinga huu –mawaziri na wazito wengine wenye umaarufu ambao unaweza kuchotwa na makapuku ombaomba wasiojulikana. Hivyo, ni juu ya wahusika kupokea tahadhari hii toka kwa mlevi mwenyewe ambaye ameshastukia dili zima. Hii nayo ni aina ya ufisadi wa kimfumo inayoanza kujengeka. Nani kawambia kuwa Kaya tajiri kama vile Marekani, Japan na Uchina yameendelea kutokana na kuombewa zaidi ya kuchapa kazi kwa juhudi na maarifi huku uwajibikaji na kutenda haki vikiwekwa mbele?
Tokana na mvuto wa maombi, si ajabu kusikia wafanya fujo wakiombea amani au wezi wakiombea haki. Hapa dawa si kuomba au kufunga bali kuacha maovu. Dawa si kuomba ni kuchapa kazi. Dawa ni kuwajibishana na kutendeana haki badala ya kuingizana mkenge. Wapo wanaoombea eti kuongezeka kwa joto, kuongezeka mafuriko, kuongezeka ubomoaji wa nyumba za mabondeni na mabalaa mengine yatokanayo na maumbile na shughuli za ngurumbili. Dawa hapa si kuomba bali kuacha kukata miti hovyo. Dawa mujarabu hapa ni kupanda miti na kutunga sheria zinazozuia uchafuzi wa mazingira utokanao na ufisadi na upogo na uwepo wa serikali mbovu kama iliyopita ambayo iliacha kila kitu kwenye autopilot.
Kesho utasikia wakiombea vijana waache kubwia madawa ya kulevya. Dawa hapa ni kuwakamata na kuwanyonga wauza unga. Mchezo huu hatari na mchafu hauishii hapa. Wapo wanaoomba kurejea kwa maadili mema. Hapa dawa si kuomba bali kupambana na uchafuzi wa maadili utokanao na ulimbukeni , miigizo, ujinga, unywanywa na ujinga. Badala ya kufungia magazeti yanayofichua maovu, fungieni magazeti ya udaku ambayo Mlevi hupenda kuyaita magazeti ya uchafu. Kwani, magazeti haya –licha ya kuuza na kusambaza ujinga na uchafuzi wa maadili sana –yamegeuza taifa letu kuwa taifa la wadaku, wambea na wapuuzi bila sababu. Nenda mkaone nchi za jirani. Hazina utitiri wa magazeti ya udaku kwa vile si mataifa ya wadaku na wapuuzi. Yote fanyeni, msije kuingilia bangi na ulabu wetu. Hatuhitaji kuombewa tuache ulabu. Kwani Mwana wa Maria aliyegeuza maji kuwa mvinyo mnadhani alikuwa njinga kama nyinyi siyo? Acha tujipigie ulabu na kututika mibangi. Kwani ndiyo nyenzo pekee tulizobaki nazo za kujiliwaza tokana na kunyonywa na kupigika kwa muda mrefu.
Wapo wanaombea hata wenye kesi kama zile za makontena bandarini ili serikali iwasahau wao na mali walizojilimbikiza. Hapa dawa ni kuiambia serikali kuwakamata, kuwafilisi na kuwanyonga. Dawa ni kufichua ajira za kujuana ambapo watoto wa vigogo wanajazwa kwenye sehemu nyeti kama Bandari, Viwanja vya ndege, Mipakani, Benki kuu, Uhamiaji, Biashara, Madini, Utalii, Mafuta na sehemu nyingine nyeti zenye ulaji wa haraka.
Mlevi yeye si bingwa wala muumini wa kuomba omba bali kusema sema hasa kuwapa vidoge wanaohitaji.
Siyo siri, tumegeuka taifa la ombaomba, wavivu na washirikina bila sababu. Huwezi kuombea amani ikawapo kama hakuna haki. Huwezi kuomba joto lipungue duniani wakati ukikata miti na kujenga kwenye vyanzo vya maji.
Huwezi kumwombea rais wakati hufuati falsafa yake ya “Hapa kazi tu”. Sidhani kama rais Kanywaji anaamini kama kuomba ni kazi zaidi ya kuchapa kazi na kuachana kuombaomba. Rais Dokta Kanywaji nakustua, unapaswa kuwastukia hawa ombaomba wa kiroho wenye uroho wa kutaka kukutumia kujitajirisha kwa njia ya kujifanyia mambo yao. Inakuwaje hawa na njaa zao waingize kaya yetu kwenye udini wao? Lisirikali halina dini na halipaswi kuwa nayo. Hivyo, halipaswi kuombewa bali kuambiwa litende haki kwa ngurumbili wote wa kaya hii ya Danganyika. Kaya yetu hahihitaji kuombewa. Wanaombewa maiti si walio hai. Kama kuomba ni dili basi kila mtu aombe kivyake na kwa imani yake. Kwanini mtulazimishe kufuata dini zetu hasa sisi ambao dini zetu ni kanywaji na si hizo zenu za kimamboleo?
Tumalizie kwa kumnukuu Bwana mkubwa Mwana wa Adamu aliyesema, “Waache wafu wazike wafu wenzao,” (Mathayo 8:22-23). Hata profesa Paulo alisema kuwa asiyefanya kazi asile. Kwani hakujua nguvu ya maombi kama ingekuwapo kweli?
Nami profesa Ayatolah, Daktari, Ustaadh Mlevi wa Mvuta bangi nasema tena kwa kinywa kipana, “Waache ombaomba wawaombee ombaomba wenzao lakini si kaya yetu.”
Chanzo: Nipashe, Januari 23, 2016.