Quantcast
Viewing all articles
Browse latest Browse all 3177

Kijiwe chamshauri Gwaijumaa aanzishe chama

         Baada ya mchunaji, sorry, mchungaji wa kujipachia uaskofu aitwaye Jose Gwaijumaa kuwafunika wanasiasa kwenye siasa, kijiwe kinahoji anafanya hivyo kama nani wakati kayani kwetu kuna utaratibu wa kutenganisha siasa na dini au anahubiri duni?
          Mpemba anaingia akiwa anavuta tasbih yake na kusema, “Wallahi mie nshangaa sana hawa UKAUA. Yaani pamoja na kumuua Pumba na Silaha bado waendelea kujiua kwa kuhubiri udini?”
          Mgosi Machungi anamchomekea Mpemba, “Hebu Ami tieeze vizui tikikueewe. Unamaanisha nini unaposema eti UKAUA wanahubii udini?”
          Mpemba anajibu, “Ami hujamsikia huyu nchunaji Jose Gwaijumaa aiyejipachia uaskofu na upupu anaomwaga ukiachia mbali madai ya ajabu aniyotoa?"
          “Ahaa unaongelea huyu msanii na mshenga wa Luwasa siyo! Nadhani anafaa sana kuvaa gwanda na si joho. Sioni tofauti yake na yule kidhabu wa nambari wani aitwaje Livingjiwe Lushindo. Hata hivyo, sishangai, msimu wa kutafunana, kuhadaana, kuuzana, kuchuuzana na kutapeliana ndiyo huu. Kimsingi, huyu Gwaijumaa alipaswa achunguzwe ukwasi wake kabla ya kujitiatia anajua siasa wakati si cha dini wala siasa ajuacho.” Anajibu Msomi Mkatatamaa.
          “Nadhani huyu msakatonge mnamuonea bure. Mshaambiwa ni mshenga. Sasa mnataka afanye kazi gani zaidi ya upambe. Je mnajua analipwa au ameahidiwa kiasi gani?” anajibu Mijjinga huku akibusu kikombe chake cha kahawa.
          Kapende anaamua kutia timu, “Nyie hamumjui huyu. Huyu ni wale wanaotumia majoho kujitajirisha. Yuko tayari kuingia kitandani na yeyote ilmradi mkono uende kinywani. Hata hivyo, siwalaumu hawa wasanii kutokana na kaya yetu kugeuzwa ya wasanii. Huoni anavyomlaumu Dk Silaha kuwa anatumiwa wakati yeye alianza zamani kutumiwa siyo kutumika?”
          Mipawa hataki aachwe nyuma. Anakwanyua mic, “Dokta Kapende nakuunga mkono na mguu. Usemayo yana maana sana. Tokana na mfumo wa kisanii, sasa hivi tuna hata wauza bwibwi wanaojiita wachungaji hata maaskofu. Ama kweli kaya imeingiliwa na mdudu huyu wa ufisadi na ulafi. Gwaijumaa akitumika basi kila mmoja anaona anatumika kama yeye!”
          Sofia Lion aka Kanungaembe anakwanyua mic, “Japo kaka zangu huwa natofautiana nanyi mara nyingi. Kwa hili mmenipata kweli kweli.”
          Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anamchokea Sofi na kusema, “Hebu tueleze vizuri nasi tukupate. Wamekupataje?”
          Huku akiwa anatabasamu Sofi anajibu, “Usipate tabu hata nawe utanipata tu. Kusema ukweli huyu kidhabu anatia kinyaa kiasi cha hata kuamsha hisia za udini. Tuliwaonya siku nyingi kuwatahadhari hawa wapingaji wa kila kitu. Sasa nadhani mnaanza kutuelewa hatimaye. Hawa ni waharibifu wala hawana lolote.”
          “Da Sofi mie nimekupata japo sivyo unavyotegemea. Yapo mambo nakubaliana nawe na yapo mengine sikubaliani nawe katu. Nadhani kama alivyosema Dk Silaha, kinyesi ni kinyesi hata kiwe chooni au chumbani. Hivyo, kwangu huyu mchunaji wala hanishangazi anachofanya. Hivi kweli kiongozi wa kiroho anaweza kuwa yule? Mmewahi kusikia lugha ya wapiga debe anayotumia? Sijui kwanini asingejiendea shule lau kujipatia elimu kuliko kuendekeza njaa! Hata hivyo, tuwalaumu hawa waliotawala kaya miaka yote kwa kulea uoza kama huu ambapo kila tapeli anawatapeli wachovu. Huyu ametumia vyote siasa na dini.”
          Kanji naye anaamua kula mic, “Mimi sangaa sana ona hii chunaji nasema ongo mingi. Mimi ona kwa TV. Eti sema bibi ya Silaa nakataza yeye siasa. Sasa veve mambo ya tandani ya Silaa sisi nahusu nini dugu yangu Jimaa?”
          Msomi anarejea, “Kuna jambo mnapaswa muelewe. Nadhani jamaa wanamng’ang’ania Dk Silaha ili waepushwe kung’ang’aniwa wao. Ukitaka kuwakwepa mbwa watupia mifupa. Kwa watu wasomi na ambao wako serious kutaka kuchukua kaya, wangejikita kuichapa nambari wani. Pia kwa watu waliopiga shule na kujua mikakati ya kisiasa wasingeruhusu wahuni na majuha kusimama majukwaani na kujadili mambo mazito wasiyo nayo ujuzi. Huyu Gwajumaa ana madhambi mengi ambayo yakiwekwa wazi kama si kukimbia kaya anaweza kuishia lupango kama si kujinyonga. Nadhani wanaojenga hisia za udini hawakosei.”
          Mzee Maneno anakula mic, “Nasikia hata hii chopa wanayoita ya Gwaijumaa kumbe si yake bali ya Luwasa anayemtumia huyu mchunaji. Hata hivyo, nawalaumi nambari wani kwa kutengeneza mazingira ya baadhi ya matapeli kuwaibia wachovu kutumia dini wakitangaza kufanya miujiza wakati miujiza yenyewe ni kuwatoa mshiko na si zaidi. Huyu Gwajumaa anapaswa achunguzwe kama kweli ni askofu, ukwasi wake na kama ana sifa anazodai anazo.”
          “Mzee Maneno maneno yako mazito sana. Nimependa pendekezo lako la kuchunguzwa akili na ukwasi wa mhusika. Kwa mtu kama yeye angefanya kama akina Rugemalayer na Singasinga wa escrow, kunyamaza akiomba Mungu itokee miujiza asinyee debe ingawa hili hawataliepuka siku moja iwe ni hapa duniani au mbinguni,” Kapende anazoza.
          “Yakhe mie nshawaambia tuunde chama vinginevyo twaweza kuwa kitu cha kupokezana baina ya matapeli wa kisiasa.” Mpemba anaonya.
          Mgosi hangoji Ami amalize. Anachomekea, “Nadhani hapa wa kuanzisha chama siyo si bai Gwaijumaa ili ahubii vizui siasa badaaa ya dini.”
          Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shangingi la Gwajumaa. Tulilikimbiza likatuacha. Vinginevyo tulitaka tunkamate na kutia adabu halafu tumvue majoho na kumvisha magwanda.
Chanzo: Tanzania Daima Sept., 16, 2015.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 3177