Hivi karibuni Jeshi la Polisi lilitoa matangazo kuonya baadhi ya wagombea kutokwenda baadhi ya maeneo. Mmojawapo aliyekumbwa na katazo hili na ambaye ameishaathirika nalo si mwingine bali mgombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) Edward Lowassa. Wengi wamehuzunishwa na kushangazwa na woga na ubabaishaji huu. Tunasema ubabaishaji kutokana na sababu zisizoingia akilini zilizotolewa na polisi. Mojawapo ya vyombo vya habari vilikariri jeshi la polisi likisema eti ziara aliyofanya Lowassa imesababisha mikusanyiko isiyo na lazima. Mikusanyiko isiyo ya lazima maana yake nini kwenye nchi ya kidemokrasia ambapo kila mwananchi anaruhusiwa kwenda atakako na kukutana na amtakaye mradi asivunje sheria?
Mbona polisi wanaongea vitu ambavyo hata njiwa pamoja na upole wake hawezi kuvumilia wala kushindwa kuvibaini kuwa ni visingizio na sababu za kitoto? Hivi kweli unaweza kuzuia mikusanyiko Dar Es Salaam wakati mikusanyiko ndiyo staili ya maisha? Hebu jiulize saa za jioni hasa wakati wa mvua pale Feri, Kariakoo na Posta Mpya kunakuwa na mikusanyiko ya maelfu mangapi ya wananchi wanaongojea usafiri kwenda makwao?
Kwa mujibu wa katiba yetu mtanzania yoyote anayo haki ya kufanya jambo lolote atakalo ilmradi asivunje sheria. Je kupiga kampeni kwa Lowassa kumegeuka kosa kisheria? Kinachogomba hapa hadi wengi wakaona kama ni woga wa serikali na uvunjaji haki za binadamu wa polisi ni ile hali ya kumzuia Lowassa wakawaruhusu wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanya yale yale wanayokataza. Mfano wa hivi karibuni kitendo cha kumzuia Lowassa kutembelea hospitali wakati mgombea mwenza wa CCM Samia Suluhu Hassan alikuwa akitembelea hospitali.
Polisi wanapaswa kutoa ulinzi sio vitisho na vizuizi kwa wanasiasa. Wawaache wanasiasa wafanye siasa zao ili umma wa wapiga kura uwasikilize na kuwapima vizuri na kuamua nani anafaa kuwaongoza. Kitendo cha polisi kinaonyesha ni namna gani CCM imeingiwa na kihoro ukiachia mbali kuwaonyesha polisi kama wanaojikomba kwa chama kilichokuwa tawala.
Pili, CCM haina sababu za msingi kuwaingiza polisi kwenye siasa zake za majitaka. Kufanya hivyo kunaweza kuleta fujo na maafa baadaye hasa ikizingatiwa kuwa wananchi wanaweza kukaidi amri haramu na kuzua vurugu kiasi cha damu kumwagika tokana na uchokozi na uvunjaji sheria huu wa polisi na serikali. Polisi na wale wanaowatumia wanapaswa kufahamu kuwa siku hizi kuna The Hague. Wanaweza kuanzisha vurugu zikaishia kwenye maafa na wanaohusika wakaishia The Hague na hayo madaraka wanayogombea wasiyapate wala kuyafaidi. Wako wapi akina Laurent Gbagbo waliojaribu uhuni huu unaoanza kufanywa na jeshi la polisi ambalo kikatiba halipaswi kufungamana na upande wowote?
Kimsingi, wanachofanya jeshi la polisi na serikali ni kuvunja katiba jambo ambalo ni kosa la uhaini kama tutaangalia sheria vilivyo bila kujali nani yuko nyuma ya jinai husika. Hivi inakuwaje mgombea wa CCM akienda hospitalini au sokoni mkusanyiko wake unakuwa wa lazima lakini wa wapinzani unakuwa si wa lazima. Hapa nani anataka kumgeuza nani juha? Tunadhani hakuna haja wala sababu ya kuwafanya watanzania mataahira wasiojua nani anawafaa au hawafai.
Polisi wawaache wanasiasa washindane kwa hoja badala ya kupendelea upando mmoja na kuhujumu mwingine jambo ambalo linaweza kusababisha hasira kiasi cha umma kusema sasa imetosha. Tumeyaona haya kwenye nchi nyingi ambazo mwisho wake yamekuwa ni machafuko. Kwanini polisi na wale wanaoitumia vibaya wameshindwa kujifunza tokana na ushenzi wa juzi nchi ya jirani ya Burundi ambako Tanzania ilijitia kwenda kusuluhisha wakati inafanya mambo yale yale.
Kama CCM wamefanya kazi yao barabara kama wanavyojigamba majukwaani, wana hofu gani na wapinzani hadi wahangaike kuingiza polisi kwenye siasa za kihalifu zinazokinzana na katiba ya nchi? Tufikie mahali tufanye mambo kama watu wazima tena wenye akili badala ya ukale na usio na faida.
Polisi nao wanapaswa kuelewa wanalipwa kwa kodi za wananchi wote bila kujali itikadi zao za kisiasa ukiachia mbali kuwa wapo hapo walipo tokana na utashi wa wananchi na siyo hao wanaotuma ambao nao ni tegemezi kwa wananchi.
Serikali inapaswa kuacha woga na unafiki wa kutangaza uchaguzi wakati huku nyuma ikiandaa hujuma kwa wapinzani. Hii nayo ni aina ya uchakachuaji inayoishushia serikali na jeshi la polisi hadhi.
Tumalizie kwa kuitaka CCM, jeshi la polisi, na serikali kucheza rafu. Kama hawataki ushindani watangaze serikali ya chama kimoja kama alivyofanya marehemu baba wa taifa Mwl Julius Nyerere na wawe tayari kupambana na athari za utwahuti huu. Pia waelewe dunia ya sasa imebadilika na watanzania kadhalika. Hatakubali kuonewa wala kuibiwa wala kuminywa haki zao za kikatiba. Ikizidi ikapungua basi polisi waunde chama cha siasa.
Chanzo: Dira Sept., 7, 2015.