Kusema ule ukweli, miaka kama mitatu kabla ya uchaguzi nilimwambia mwanafunzi wangu aishie Toronto kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa na mgombea mmoja wa maana na anayeuzika, Dk John Pombe Magufuli. Tarehe 26 Agosti 2015 majira ya saa kumi hivi za huku alinipigia simu akitaka nimwambie nilijuaje siri hii. Sitaki kujifanya mtabiri au waganga njaa wanosema walioteshwa. Sikuoteshwa zaidi ya kusoma uoza wa CCM. Hivyo, nilimjibu mwanafunzi wangu kuwa kama ningekuwa mbunge au waziri, basi ingekuwa mimi au Magufuli. Mwanafunzi wangu wa zamani alicheka sana na tukaachia hapo.
Japo sishabikii siasa za Tanzania kutokana kuwa mbali, hakuna mtu niliykuwa namwanimi kama Magufuli. Hata siku chache kabla ya CCM kuteua na kupitisha mgombea wake, niliandika makala kwenye gazeti la Dira yenye kichwa cha “Wapinzani wamuangalie sana Magufuli” Nakumbuka nilituma makala hiyo Julai 11. Nataka kuonyesha ni jinsi gani Magufuli alikuwa amejijengea umaarufu kutokana na uchapakazi wake na kutokwa na makundi wala kutumia fedha kutafuta madaraka. Kwangu huu ulikuwa ni ushahidi kuwa Magufuli si mwenye tamaa ya madaraka na anaweza kuwafaa wananchi.
Pamoja na kusema yote hapo juu, matamshi ya Magufuli –kama alivyokaririwa na vyombo vya habari siku moja baada ya kuongea na mwanafunzi wangu –yameanza kufanya nibadili mwelekeo. Je baada ya kuaminiwa na CCM Magufuli ameanza kubadilishwa na mfumo hata kabla ya kuingia madarakani ambapo tulitegemea angeubadili huu mfumo? Sitaki niulize maswali mengi. Ninachotaka kusema hapa ni kumshauri Magufuli aangalie aendako na kufahamu kuwa safari ya kisiasa inaweza kuwa ndefu hata kama inagharimu masaa kama ilivyotokea kwa mpinzani wake mkuu Edward Lowassa ambaye aliingia kwenye ukumbi wa kuteua na kupitisha mgombea wa CCM akiamini kuwa hakuwapo mwingi isipokuwa yeye akaishia kutimkia upinzani.
Nitatoa nukuu mbili za Magufuli ambazo zinaweza kumuonyesha kama rais asiyefaa hivyo kuwashawishi wananchi wasimchague. Akiwa mkoani Katavi alikaririwa mara mbili akisema, “Naowaombeni jamani, hatuchagui malaika, kila mtu ana Tatizo Lake. Inawezekana wengine tumechoka hata kumwangalia, lakini mkitaka nifanye kazi vizuri nileteeni bwana huyu,”
Magufuli alikuwa akimtetea Joseph Kandege aliyeonekana kuchokwa na kuchukiwa na wananchi wa jimbo la Kalambo mkoani Katavi. Je hapa tunajifunza nini? Je inakuwaje Magufuli akatetea watu wabovu kama kweli naye si mbovu?
Hebu angalia nukuu nyingine, “Wewe nenda hata kama humpendi fumba macho lakini umpigie nani?” Wananchi walijibu, “Malochaa.” Magufuli aliyasema hayo kwenye Kijiji cha Laela. Magufuli alikaririwa akimtetea Ignas Malocha, mbunge mwingine aliyeonekana wazi kuchukiwa na wale waliomchagua akaishia kuwasaliti na kuwaangusha. Kwanini Magufuli anawashauri wapiga kura vitu visivyoingia akilini? Akiwa Mkoani Sumbawanga alimtetea mbunge mwingine ambaye amebanwa Hilary Aeshi.
Kwanini anawashauri watu wawachague watu wanaowachukia kutokana na uoza wao kama siyo kuwahujumu? Cha msingi hapa ni wahusika kujua kuwa huo mzigo na gamba anavyotetea Magufuli vitakapoanza kuwaumiza, watakaoumia ni wao na si Magufuli. Kimsingi anachobainisha Magufuli ni kwamba hata hiyo mizigo itakapoanza kuvuruga na kuvurunda atailinda kwa kutumia rungu lake la urais. Je wananchi wapewe ishara gani kuwa wanahujumiwa na wale waliowategemea; hivyo wachukue hatua? Anachobainisha Magufuli ni kufuata nyayo za Jakaya Kikwete ambaye aliwakingia kifua watu kama Benjamin Mkapa, familia yake na marafiki zake hata walipobainika kujitwalia na kuiba mali za umma kama vile Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira na wale wote walioghushi. Mtu wa namna hii ni kwa kuogopwa kama ukimwi kama siyo ukoma.
Tunapenda kuhitimisha makala hii tukimshauri Magufuli asichafue rekodi yake kwenye majukwaa. Oktoba siyo mbali na wananchi watakuwa bado wanakumbuka maneno yake. Hata hivyo, ashukuru Mungu kuwa wapinzani hawachambui vilivyo kauli zake na za wana CCM wenzake kama upupu wa juzi aliomwanga rais mstaafu Benjamin Mkapa ambaye alijivua nguo hadharani huku akitoa matusi yanayoweza kumharibia Magufuli. Kweli binadamu si malaika. Makosa aliyotenda Katavi asiyarudie vinginevyo ataanza kujionyesha tofauti na tulivyomdhania. Mchapakazi wa kweli anapaswa awatake wananchi wampe wachapakazi hata kama wanatoka kwenye upinzani. Hii itamuonyesha kama mtu anayetaka maendeleo na si siasa za kipuuzi za kulindana kama tulivyozishuhudia.
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 6, 2015.