Kila mpenda mageuzi na haki angetamani Chama Cha Mapinduzi (CCM) kishindwe kwenye uchaguzi ujao au hata kikishinda siyo kwa kishindo kama kilivyiozea. Baada ya waziri mkuu wa zamani aliyeachia ngazi kwa shinikizo la kubainika kushirika kashfa ya Richmond, Edward Lowassa kujiunga na upinzani, alizua mtafaruko ambapo wapo walioona kama ni neema kwa mageuzi na pia walioona kama ni laana kwa upinzani.
Kadiri siku zinavyokwenda, upande unaopinga kujiunga kwa Lowassa na upinzani unazidi kupata mashiko huku nchi ikitikisika si kidogo. Kwa hesabu za haraka haraka ni kwamba katika mtanange huu wanaoonekana kunufaika ni CCM hasa ikizingatiwa kuwa sintofahamu baina na miongoni mwa kambi ya upinzani vinawapa nafuu. Maana, wengi walidhani wapinzani wangeshupalia maovu ya CCM badala ya kugeukana na kukimbiana wao kwa wao. Je hapa kosa ni la nani?
Wapo wanaolaumu upinzani kwa kumpokea Lowassa na kumpa kila alichotaka huku wenyewe ukionekana wazi kukosa kile ulichojiandalia. Mfano, Profesa Lipumba alikaririwa akisema kuwa dhamira na nafsi vyake vilimsuta hasa baada ya kugundua kuwa UKAWA walishindwa kusimamia maadili waliyokuwa wakiyatetea. Alisema kuwa alishangaa kuona wale waliouzuia kuandikwa kwa katiba mpya ya wananchi ndiyo wamegeuzwa waleta mageuzi yale yale waliyozuia na kuua. Hapa, Lipumba ana hoja. Amejitahidi kifalsafa kuonyesha yuko upande gani.
Hata hivyo, Lipumba aliwachanganya wengi pale alipokiri kuwa alishiriki mchakato mzima wa kumpokea na kumkweza Lowassa. Wengi wanashangaa kwanini sasa na si wakati ule au kuna mkono wa mtu? Kwa siasa za Tanzania lolote linawezekana. Swali kubwa linaloulizwa ni: Je kuna kitu au vitu UKAWA wanaficha juu ya kukubaliana kum-import Lowassa?
Iweje mtu mzima, msomi na mwenye akili timamu ashiriki mchakato halafu aupige teke baada ya kukamilika kama hakuna namna? Je kuna kitu kimetembea hapa au ahadi ambazo zimewaacha wengine nje? Maana ukiangalia mantiki ya kumpa Lowassa tiketi haraka haraka bila hata kushauriana na wanachama unashangaa kila kitu. Je kujiondoa kwa Lipumba ni jambo la kawaida ingawa kuhama vyama kwa wanasiasa ni jambo la kawaida? Nadhani kuna tofauti kidogo hasa ikizingatiwa kuwa Lipumba hakuwa anapambana na upinzani ndani ya chama chake wala hakuwa akigombea cheo kingine kama vile ubunge kiasi cha kulazimika kuhama ili kufanikisha alichokitaka. Lazima kutakuwa na jambo tena kubwa tu ambalo wahusika hawataki kuliweka wazi. Maana, kama ni kusutwa na dhamira na nafsi, ilibidi kutokee siku Lipumba alipopokea taarifa ya kuwepo mpango wa kumkaribisha na kumpokea Lowassa. Je kuna ahadi za vyeo ambapo wapo walioahidiwa unono wakati wengine wakiachwa nje? Maswali ni mengi kuliko majibu.
Baada ya Lipumba kujiuzulu, wasioona mbali wameanza kumuandama wasijue ngoma bado mbichi. Je kama kuna yaliyofichika na Lipumba akasongwa na akaamua kuyaweka hadharani, upinzani utakuwa na lake hapa? Je kuondoka kwa Lipumba kutawapa wangapi moyo kufanya maamuzi magumu kama haya? Je jibu la kuondoka Lipumba ni ubabe au busara zaidi na kuheshimu mchango wake kwenye kulea na kukuza upinzani?
Hata hivyo, kujiuzulu kwa Lipumba na ile sintofahamu inayoendelea kuhusiana na mustakabali wa Dr Wilbrod Slaa kwenye chama chake ni ushahidi tosha kuwa vyama vyetu bado si huru. Bado ima vinamilkiwa na waanzilishi au ndugu zao au watu wao au bado vinaendeshwa kichama kimoja. Maana, kama kungekuwa na uhuru na demokrasia ya kweli, tungesikia nukta ambapo wahusika wameshindwa kukubaliana au kukubaliana. Ukiangalia wazungumzaji wakubwa katika sakata hili, unashangaa kugundua kuwa wahanga wa ujio wa Lowassa walikuwa wemevishwa kilemba cha ukoko wakati wanaoendesha vyama wako nyuma ya pazia. Nataka anayeona dhana hii ni potofu anipe mantiki ya Lipumba na Slaa kuonekana kama wasio na thamani wala mamlaka ikilinganishwa na wengine. Je wapo wenye vyama wanaovuta kamba nyuma ya pazia? Je vyama vya namna hii vinaweza kutuvusha au kufanya mambo tofauti na CCM?
Laiti Lipumba angeyasema yote yaliyomkwaza hadi akajipiga mtama hasa ikizingatiwa alivyokiri kuwa alishiriki mchakato mzima lakini akaupiga chini kwenye saa za mwisho. Laiti na Slaa angefanya maamuzi magumu na kueleza kila anachojua, huenda wananchi wangepata faidi kwa kujua sura hali ya upinzani wetu ambao kipindi hiki umejitahidi kujionyesha ulivyo sawa na CCM.
Ukitathmini uzito wa Lipumba kama mwenyekiti wa chama na nguzo mojawapo ya UKAWA na sintofahamu ya Dk Slaa, unagundua kuwa mizani inalalia upande wa UKAWA. CCM wamempoteza Lowassa ambaye tokana na alivyokwishachafuka angewapa kibarua kigumu kumsafisha wakati UKAWA wameondokewa na kiongozi wa chama tena asiye na tuhuma hata moja. Lowassa hakuwa mwenyekiti wa chama wala mwenye ushawishi mkubwa serikalini baada yakupoteza uwaziri mkuu. Tayari alikuwa majeruhi ambaye CCM wakiamua kupiga kwenye donda atajeruhika zaidi kiasi cha kuzua wasi wasi kuwa anaweza kuzama na upinzani wote jambo ambalo –Mungu apishe –mbali ni hasara kwa mageuzi nchini. Hata akishinda ana jipya gani ambalo CCM hawana? Inashangaza ni kwanini upinzani hakuliona hili kiasi cha kujiweka rehani kwa Lowassa kana kwamba yote uliyokuwa ukisema ili kuwa ni danganya toto au changa la macho. Haiwezekani watu waliojiandaa miaka yote hii watundike daruga kwa mtu mmoja huku wakiwa tayari hata kusambaratika bila kueleza kilichopo nini cha mno.
Tumalizie kwa kuwataka wahusika wazidi kutupa mwanga juu ya kuendelea kuvunjika kwa ndoa yao huku mchumba mpya akipeta bila maelezo pamoja na mapungufu yake.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 16, 2015.